KAMA ulizoea kuwaona jukwaani wanamitindo wa kiume Calisah, Chris Mziwanda, Daxx na wengine wengi wakifanya yao, basi tambua kwamba kuna wacheza mpira wa miguu nao wanaiweza shughuli hiyo.
Dickson Job wa Yanga na John Bocco kutoka JKT Tanzania, wanajulikana kwa watu kuwa ni wacheza mpira wa miguu mahiri lakini kumbe wapo vizuri katika jukwaa la mitindo.
Wanasoka hao Novemba 20, 2024 walionekana wakipita Jukwaa la Usiku wa Madini katika tukio lililofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Job ambaye pia amewahi kuitumikia Mtibwa Sugar akicheza nafasi ya beki wa Yanga SC wakati Bocco ni mshambuliaji wa zamani wa Azam na Simba, walitumika kutangaza madini mbalimbali yapatikanayo Tanzania katika tukio hilo lililowakutanisha watu kutoka mataifa tofauti.
Mwanaspoti ilipata nafasi ya kuzungumza na wachezaji hao kwa nyakati tofauti kutaka kufahamu ilikuwaje wakafanikiwa kuwepo katika tukio hilo wakiwa ni sehemu ya wahusika wakati wamezoeleka katika kucheza mpira wa miguu.
“Kuwa mchezaji mpira sio kwamba unashindwa kufanya vitu vingine, kikubwa ni kujiamini na kujitambua kuwa unaweza kufanya kitu chochote ukihitajika, hivyo mimi nilipohitajika kufanya hivi nikalipokea kwani ni kitu cha kutangaza nchi yetu,” amesema Job ambaye hivi karibuni alikuwepo katika kikosi cha Taifa Stars kilichofuzu Afcon 2025.
Kwa upande wake Bocco amesema: “Sikuwahi kufanya umodo sehemu yoyote, hii ndio mara yangu ya kwanza, na kama umeaminishwa unaweza kufanya basi sikusita nikakubali na nikasema nitaweza sababu sikuona ugumu wowote ukizingatia ni jambo la kitaifa.”
Mbali na wachezaji hao, walikuwepo pia walimbwende Hamisa Mobetto, Miss Tanzania 2024 Halima Kopwe, Miss Grand Fatma Suleiman na wengineo ambao walitumika kunadi madini yapatikanayo Tanzania.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hatua ya kutumia watu hao maarufu ni kutokana na ukweli kwamba Tanzania imejaaliwa na utajiri mkubwa ambao mataifa mengine yanapaswa kuwafahamu na kuwavutia kuwekeza nchini kwenye sekta ya madini.
Usiku wa Madini ni mwendelezo wa matukio ya mkutano wa 6 wa madini kitaifa na uwekezaji katika sekta ya madini.
Mbali na shoo ya uanamitindo, kwa upande wa burudani ya muziki ilipambwa na Banana Zorro akiwa na bendi yake ya B Band.