Songea. Polisi mkoani Ruvuma wanawashikilia watu wawili akiwamo mfanyabiashara wa dawa za mifugo, Nickson James (29) mkazi wa Mtaa wa Buswelo, Manispaa ya Ilemela Mwanza, kwa tuhuma za kusafirisha dawa bandia za mifugo za Sh78.99 milioni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Novemba 24, 2024 ofisini kwake mjini Songea, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya amesema watu hao walikamatwa Novemba 7 mwaka huu saa 6:30 mchana katika kijiji cha Lilondo, Kata ya Wino, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
“Siku hiyo, askari walikamata gari aina ya Toyota DYNA lenye namba za usajili T 185 EBX lililokuwa likisafirisha dawa hizo kutoka Songea kuelekea Njombe. Gari hilo, lililokuwa likiendeshwa na Frank Ndunguru,” amesema.
Kamanda Chilya amedai kuwa, baada ya kukamatwa kwa gari hilo, uchunguzi ulifanywa kwa kushirikiana na wataalamu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na ikabainika kuwa dawa hizo zimeingizwa nchini kinyume cha sheria kupitia njia zisizo rasmi, huku baadhi zikiwa bandia na nyingine zikiwa chini ya viwango.
Amezitaja dawa zilizokamatwa ni Levimox Super, Alben Blue, Oxysol Plus, Bisol, Piperazine, Tylodoxy 200 na Vetoxy 20 zenye thamani ya Sh51,174, 599.
Ametaja dawa nyingine ni aina ya Hi-tet, Levafas Diamond na Oxy-met 10 inj (500ml & 250ml) zikiwa kwenye chupa 1,026 na madumu 12 zenye thamani ya Sh19.456 milioni.
“Dawa ambazo zimesajiliwa lakini hazina kibali cha kuingia nchini ni Ivermed, Ascarex na Polytricin,” amesema Kamanda Chilya.
“Hizi zilikuwa chupa 512 na pakiti 92 zote zikiwa na thamani ya Sh8.355 milioni.”
Kamanda Chilya amesema upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka husika, huku jalada la kesi likiwasilishwa ofisi ya mashtaka mkoani Ruvuma kwa hatua zaidi za kisheria.
Dickson Mapunda amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuzikamata dawa hizo kabla hazijaingia sokoni.
“Hawa watu wanataka kutuzidishia umasikini tu, mtu una mifugo yako michache badala ya kuimarisha wao wanatuletea dawa feki za kuwatibu, naomba sheria ichukue mkondo wake,” amedai Mapunda.
Agnes Nkondola, ameiomba Serikali isiishie kukamata tu, bali ifanye upekuzi kwenye maduka ya dawa za mifugo, huenda dawa hizo zipo.