YANGA chini ya bosi mpya, Sead Ramovic inarudi uwanjani kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na mashabiki wa timu hiyo wanataka kuona kuna kitu gani kocha wao amekiongeza, lakini mwenyewe ametuma salamu akisema kwenye timu yake hataki kuona mpinzani anapumua na wataanza na Al Hilal.
Akiwa amekaa na timu hiyo kwa siku nane tangu aanze kazi, Ramovic ambaye amechukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyeachana na Yanga baada ya matokeo mabaya, ameanza kuingiza vitu vyake anavyoamini vinaweza kuibeba timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa pamoja na Ligi Kuu Bara.
Katika mazoezi yake yaliyoshuhudiwa na Mwanaspoti, amekuwa anataka kuona wachezaji wake wakicheza soka la kasi zikipigwa pasi za haraka kwenda mbele na mara kwa mara akiwataka kutumia nafasi wanazopata, lakini amekuwa akiwasisitiza kuutafuta mpira haraka sana wanapoupoteza.
Baada ya mazoezi hayo, Ramovic aliliambia Mwanaspoti ingawa bado ana siku chache katika timu hiyo, hawezi kubadilisha mambo mengi sana lakini anataka kuona timu yake inacheza soka la kushambulia, kuufanya mpira utembee na wasiwape wapinzani nafasi ya kujiuliza.
Ramovic alisema falsafa ya soka lake hataki kuona mpinzani anapumua sawasawa akitaka kuona wachezaji wake wanashambulia kwa nguvu kwa wakati wote huku wakiwa na nidhamu ya kukaba.
“Aina hii ya soka inahitaji utimamu mkubwa wa mwili kwa wachezaji wetu na itahitaji muda, lakini naamini muda ukifika huko mbele tukiiva kwenye hili itawaimarisha wachezaji wetu mmoja mmoja na timu itakuwa kwenye ubora mkubwa, kwa sasa tunachotaka ni kucheza kwa kasi, kuwasumbua wapinzani wasiwe na muda wa kupumua kujiuliza wamekosea wapi,” alisema Ramovic.
“Unajua unaweza kwenda gym leo ukanyanyua vyuma lakini huwezi siku inayofuata ukawa umeshafanikiwa kutunisha misuli, lakini kuna hali ya utofauti ya mwili utaisikia na hiki ndicho tunakifanya sasa. Kuna baadhi ya vitu tunaweza kuviona vinaanza kubadilika lakini tunapotaka tutahitaji muda, tukifanikiwa tunachofanya sasa hakika matokeo yetu yatakuwa mazuri,” alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.
Aidha Ramovic ‘amevimba’ akisema anaamini ni kocha sahihi kwa Yanga na anataka kuona timu hiyo inaendeleza mafanikio yake katika utawala wake.
“Kwangu mimi ni kocha sahihi kwa hii klabu, tuna jukumu moja kubwa la kuendeleza mafanikio ya hii klabu, tutafanya kazi kwa nguvu ili tufikie malengo, nafahamu aina ya ugumu ambao tutakwenda kukutana nao mbele ya wapinzani wetu Al Hilal lakini tutajitahidi kutumia ubora wa wachezaji wetu na ufundi kupata matokeo mazuri.”
Yanga inaingia uwanjani kesho kuvaana na Al Hilal katika mchezo wa kwanza wa kocha huyo, ukiwa ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, Yanga ipo Kundi A pamoja na Al Hilal, TP Mazembe na MC Alger.