Nairobi. Naibu Rais aliyetimuliwa madarakani nchini Kenya, Rigathi Gachagua amedokeza kurejea kwa kishindo kwenye siasa Januari 2025, akisema msuguano wake na Rais William Ruto umemsaidia kumjua ni mtu wa aina gani.
Akizungumza wakati wa misa takatifu mjini Murang’a jana Jumapili Novemba 24, 2024 Gachagua amesema kuwa mgogoro wake na Rais Ruto umemruhusu kupanga upya mikakati yake ijayo ya kisiasa.
Kwa mujibu wa The Citizen Digital, Gachagua amesema kwamba alibaini rasmi Rais Ruto ni mtu wa aina gani ilipodhihirika alichangia kuondolewa kwake.
“Sisi kama watu wa Mlima Kenya tunachukia mambo mawili; uongo na usaliti. Januari ijayo baada ya mazungumzo tutatoa mwelekeo wetu. Hatutajikuta tena kwenye shimo tulimo,” amesema Gachagua.
“Rais Ruto, rafiki yangu, alifanya jambo jema kuleta vita hivi dhidi yangu na watu wa mlimani kwa sababu sasa tunamjuana tutakuhutubia jinsi tunavyokujua wewe ni nani. Sasa tutakuwa na mazungumzo kwa heshima.” ameongeza
Ruto afunguka sakata la michango kanisani
Rais wa Kenya, William Ruto ameshikilia msimamo wake kuwa hatoacha kutoa misaada ya kifedha kwa makanisa licha ya ukosoaji mkubwa kutoka kwa viongozi wa dini nchini humo.
Akizungumza jana Jumapili Novemba 24, 2024 kwenye ibada mjini Kericho Rais Ruto alibainisha kuwa amejitolea kuunga mkono maendeleo ya makanisa na kuenea kwa Ukristo kwa kutoa pesa.
Ruto amesema hatasitisha kuendeleza utamaduni wake kwa vile amezoea kutoa na kuongeza kuwa hatanyamazishwa na wachochezi.
“Hatuna msamaha kabisa tunapomtolea Mungu kwa sababu Mungu alitoa kwanza, tunalielewa neno la Mungu kiasi cha kujua kwamba ni heri kutoa kuliko kupokea na ndicho tunachokwenda kufanya.”
“Tutajenga makanisa yetu na tutashirikiana kueneza neno la Mungu. Nimesaidia kujenga makanisa 30 ndani ya miaka 30 na sijawahi kukosa maana najua siri ya kutoa na najua inafanya nini,”amesema.
Ikumbukwe Novemba 17, mwaka huu Kanisa Katoliki nchini Kenya lilirudisha sadaka ya fedha za Kenya Sh6 milioni (Sh123 milioni) zilizotolewa kwenye ibada ya Jumapili na Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, huku likiwataka viongozi wa kisiasa waende kanisani kupewa chakula cha kiroho na si kutafuta umaarufu.