KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema mashabiki wa timu hiyo watarajie mchezo mzuri wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati kikosi hicho kitakapopambana keshokutwa Jumatano dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola.
Miamba hiyo iliyopangwa kundi A, sambamba na timu za CS Constantine ya Algeria na CS Sfaxien kutoka Tunisia, zitakutana katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi utakaopigwa saa 10:00 jioni, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Tunaenda kucheza na mpinzani mgumu ambaye sisi benchi la ufundi na wachezaji kiujumla tunawaheshimu, ni mechi nzuri na muhimu kwetu tunayoiwaza zaidi hivyo, niwaombe mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kutupatia motisha ya kufanya vizuri,” alisema Fadlu raia wa Afrika Kusini.”
Fadlu alisema anategemea mchezo mgumu kutokana na aina ya wapinzani wanaoenda kukutana nao ingawa wao kama benchi la ufundi na wachezaji wamejipanga kuonyesha uwezo mzuri, ili kuanza kampeni vizuri za michuano hiyo wakiwa uwanja wao wa nyumbani.
“Tutashambulia kwa nguvu zetu zote ili kupata matokeo chanya tofauti na mchezo uliopita na Pamba Jiji ambao hatukuweza kufanya hivyo kutokana na aina ya uwanja kutoruhusu huu ni mchezo wa kupata ushindi na tayari wachezaji wangu nimeshawaandaa vyema.”
Mmoja wa watu wa karibu na klabu hiyo kutoka Angola ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake gazetini aliliambia Mwanaspoti, Simba inapaswa kumlinda kiungo mkabaji wa kikosi hicho, Francisco Matoco kutokana na ubora wake wa kuusoma vyema mchezo.
“Ni mchezaji mzuri sana ambaye Simba wanapaswa kuhakikisha wanamlinda ili asiweze kuwaletea madhara, ni hatari na anajua kusoma wapinzani uwanjani kwa haraka na kuunganisha timu hivyo, wawe makini naye,” alisema mmoja wa watu kutokea Angola.
Chanzo hicho kilisema, Bravos sio timu ya kutisha sana ukilinganisha na Simba ambayo tayari imeshajijengea ufalme katika soka la Afrika, ingawa hawapaswi kuwadharau kwani wapinzani hao wanacheza kitimu zaidi ndio maana wamefika hapo walipo.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bravos, Faustino Lemos alisema timu hiyo inatarajia kuingia nchini Tanzania kesho Jumanne mapema, huku ikiwa na msafara wa watu 43, wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki zao kutoka Angola.
“Sio wageni tena hapo nchini Tanzania kwa sababu tulishakuja hivi karibuni tulipocheza na Coastal Union, siwezi kueleza tutakuja na mpango gani safari hii, ila tunatambua tu ni mechi nyingine ngumu na muhimu kwa kila upande,” alisema Lemos.
Francisco ni kiungo mzuri ndani ya timu hiyo ambapo Simba inapaswa kumchunga kwani amefunga mabao mawili kati ya sita ya kikosi hicho katika hatua za awali za kufuzu makundi ya mashindano hayo, jambo linaloonyesha wazi ubora na uwezo wake.
Timu hizo zinakutana zikiwa na matokeo mchanganyiko katika Ligi zao ambapo Simba ilitoka kuifunga Pamba Jiji FC bao 1-0, huku kwa upande wa Bravos ikitoka suluhu mechi yake ya mwisho kwenye Ligi Kuu ya Angola ‘Girabola’ dhidi ya Academica.
Simba iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 28, baada ya kucheza 11, imeshinda tisa, sare mmoja na kupoteza mmoja, ikifunga mabao 22 na kuruhusu matatu, ikiwa na wastani mzuri tofauti na wapinzani wao katika kundi lake.
Kwa upande wa Bravos katika Ligi Kuu ya Angola ‘Girabola’ imecheza michezo 12 ambapo kati ya hiyo imeshinda mitatu tu, sare saba na kupoteza miwili, ikiwa nafasi ya tano na pointi 16, nyuma ya vinara, Petro Atletico iliyokusanya pointi 23.
Katika michezo hiyo kikosi hicho kimefunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10, jambo linaloonyesha wazi hakipo vizuri katika maeneo mawili ya ushambuliaji na uzuiaji, kitu kinachoweza kuipa faida Simba itakapokutana nayo.
Bravo inarejea tena jijini Dar es Salaam kwa mara ya pili msimu huu baada ya hatua ya awali kutoka suluhu na ‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union hivyo, kufuzu kwa jumla ya mabao 3-0, kufuatia mechi yake ya kwanza ikicheza Angola kushinda kwa 3-0.
Baada ya hapo kikosi hicho kikakutana na FC Lupopo ya DR Congo ambapo kilishinda kwa jumla ya mabao 3-1, kufuatia mchezo wa kwanza jijini Angola kushinda bao 1-0, kisha mechi yake ya marudiano iliyopigwa huko Congo kikashinda tena mabao 2-1.