Waathirika wa mafuriko Ifakara warejea kwenye makazi yao

Ifakara. Waathirika 160 kati ya 400 wa mafuriko waliowekwa kwenye kambi ya Shule ya Msingi Ifakara wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro, wamerejea kwenye makazi yao huku wakiendelea kufanya ukarabati wakati Serikali ikikagua hali ya usalama wa nyumba hizo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Mei 8, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya amesema baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko, hali ya hewa inaonekana kuwa nzuri na maeneo mengi yaliyojaa maji yameanza kukauka.

“Leo tunashukuru Mungu jua linawaka na maeneo mengi yaliyokuwa yamejaa maji jana yameanza kukauka, tulikuwa na waathirika kama 400 hivi tuliowahifadhi pale Shule ya Msingi Ifakara, lakini baada ya hali ya hewa kukaa vizuri, wameanza kurejea kwenye makazi yao na wengine waliamua kukimbilia kwa ndugu zao, haya maji ya Ifakara ni ya kupita,” amesema Kyobya.

Kuhusu miundombinu, amesema zipo barabara na makaravati yanayounganisha vijiji na kata zimekatika, hata hivyo, Serikali kushirikiana na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini  (Tarura) wanaendelea kufanya tathimini ya uharibifu huo.

Mratibu wa kamati ya maafa ya Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Jafari Ngogomela amesema moja ya kazi inayofanywa sasa na kamati hiyo ni kutoa elimu ya afya ili kuepuka magonjwa ya mlipuko na pia kutoa tahadhari kwa wananchi kutovuka kwenye mito.

“Kwa sasa vyoo vingi vimepasuka na vinyesi vimetapakaa kwenye tabaka la juu la ardhi, hivyo tunawatahadharisha wananchi kuchukua hatua kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na kuhimiza kuchemsha maji ya kunywa,” amesema Ngogomela.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliokumbwa na mafuriko, Diwani wa Viwanja sitini, Erick Kulita amesema pamoja na mvua kukata, bado mito imejaa maji hivyo amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

“Haya maji ni mengi na watoto wanaona kama sehemu ya kucheza, wazazi wasipokuwa makini wanaweza wakazama, wazazi wenzangu tuwe karibu na watoto wetu katika kipindi hiki cha mvua,” amesema Kulita.

Related Posts