Matokeo ya kufungana mabao 2-2 waliyopata Singida Black Stars dhidi ya Tabora United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo Novemba 25, 2024 kwenye Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi mkoani hapa, yameikwamisha timu hiyo kukaa nafasi ya pili kwenye msimamo badala yake imesalia nafasi ya nne ikifikisha alama 24.
Mchezo huo umechezwa leo saa 4:00 asubuhi baada ya kuahirishwa jana kutokana na sababu za hali ya hewa.
Singida Black Stars walitangulia kupata mabao yao kupitia kwa Elvis Rupia dakika ya 16 na Anthony Tra Bi Tra (dk 32). Tabora United ilisawazisha kwa mabao ya Yacouba Songne dakika ya 45+1 na Heritier Makambo (dk 49).
Yacouba alionekana kuishughulisha vilivyo safu ya ulinzi ya Singida Black Stars ambapo licha ya kiwango bora alichoonyesha lakini alishindwa kumaliza mchezo baada ya kuumia na kulazimika kutolewa dakika ya 68, hata hivyo ndiye alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.
Kocha Mkuu wa Tabora United, Anicet Kiazayidi raia wa DR Congo amesema pointi moja waliyopata mbele ya Singida Black Stars haikuwa rahisi.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kujitoa na kupata alama moja kwenye uwanja wa nyumbani, tulianza mchezo tukiwa na morali ya chini ndio maana tulifungwa mabao mawili ya haraka lakini baadae tulikazana na kusawazisha, hivyo tunashukuru kwa yote,” alisema na kuongeza.
“Wapinzani wetu Singida Black Stars walikuwa vizuri, licha ya kipindi cha pili licha kuwamiliki eneo la kiungo kwa kiasi kikubwa lakini wametupa upinzani mkubwa, hivyo makosa tuliyofanya leo tutayafanyia kazi kwani mchezo ujao dhidi ya KMC tunatakiwa kushinda kwa nguvu zote tukiwa ugenini.”
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Mbelgiji Patrick Aussems amesema nafasi walizoshindwa kuzitumia zimewafanya wakose alama tatu.
“Tulikua na mchezo mzuri leo dhidi ya Tabora United ndiyo maana tumetangulia kufunga, lakini wapinzani wetu waliamka na kusawazisha, ndio soka, lakini makosa ya leo tutayafanyia kazi ili mchezo ujao na Azam tuweze kufanya vizuri zaidi.
“Tumetengeneza nafasi nyingi kwenye mchezo huu lakini umakini umetugharimu kupata matokeo mazuri, hivyo tunayo kazi ya kufanya kwani malengo yalikuwa ni kushinda ili tupande kwenye nafasi za juu zaidi kwenye msimamo wa ligi,” alisema Aussems.
Baada ya matokeo hayo, Tabora United wamepanda nafasi moja kutoka ya sita hadi ya tano baada ya kucheza mechi 12 na kukusanya alama 18 ikiishusha Fountain Gate yenye alama 17.