Watu tisa wa familia moja wamefariki dunia baada ya nyumba walizokuwa wakiishi kusombwa na maji baada ya mto uliopo jirani na makazi yao kujaa maji, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Tarime.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Novemba 25,2024 katika Mtaa wa Bugosi, Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara ambapo miili ya watu hao ilisombwa hadi ndani ya mto Mori uliopo jirani na makazi yao.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele amesema hadi sasa miili saba imekwishaopolewa kutoka mtoni na utafutaji wa miili mingine unaendelea kwa kushirikisha vyombo vya uokoaji na wenyeji wa eneo hilo.
Amesema katika tukio hilo watu wawili wamenusurika ambapo mbali na vifo hivyo, pia limesababisha uharibifu wa mazao yaliyosombwa na maji hayo na mali.
Endelea kufuatilia Mwananchi.