DK. Fredy Rutachunzibwa wa Kairuki hospitali ambaye ni Mtanzania wa kwanza kufuzu mafunzo ya kutibu saratani kwa kutumia teknolojia ya HIFU (High-Intensity Focused Ultrasound), ameeleza namna tiba hiyo inavyotolewa bila upasuaji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
HIFU ni teknolojia ya kisasa inayotumia mawimbi ya sauti yenye nguvu kuteketeza seli za saratani kwa usahihi, bila kuhitaji upasuaji.
Akizungumza na gazeti hili jana, daktari huyo alisema mbinu hiyo inapunguza maumivu, hatari ya maambukizi na muda wa kupona kwa wagonjwa.
Alisema Hospitali ya Kairuki ni ya kwanza nchini Tanzania, Afrika Mashariki na Kati kutumia teknolojia ya HIFU, na ni ya tatu Barani Afrika.
Alisema teknolojia hiyo inatoa suluhisho kwa wagonjwa wengi wa saratani, hasa wale wanaokosa matibabu ya kisasa kutokana na vikwazo vya kifedha au umbali wa hospitali.
Dk. Rutachunzibwa ambaye alipata mafunzo hayo nchini China mwaka jana alisema matibabu kwa kutumia HIFU hayaingizi chochote ndani ya mwili.
“Ngozi haiguswi na hakuna kidonda kinachotengenezwa, hakuna nusu kaputi yaani mgonjwa anaondolewa uvimbe huku akiwasiliana na daktari anayemhudumia,”alisema na kuongeza
“Kinachofanyika ni kwamba mawimbi sauti yanapelekwa katika eneo lenye uvimbe unaunguzwa bila kuathiri sehemu zingine na matibabu haya yanatolewa kwa wenye saratani za aina mbalimbali,” alisema
Alisema HIFU inaboresha huduma za afya kwa kuongeza ufikiaji wa matibabu ya kisasa na kupunguza vifo vinavyosababishwa na saratani nchini Tanzania.
“Teknolojia hii ni hatua muhimu katika mapinduzi ya sekta ya afya nchini kwasababu matibabu haya walilazimika kuyafuata mataifa yaliyoendelea lakini sasa ayanapatikana hospitali ya Kairuki,” alisema.