Mohamed Abdel Rahman amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Al Hilal akiwa ameisadia klabu yake kupata ushindi kwenye michezo muhimu ya ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msimu huu Abdel Rahman amecheza mechi nne ambapo amefunga mabao matatu kwenye Ligi Kuu ya Mauritania ambayo Al Hilal inashiriki baada ya Ligi Kuu Sudan kusimama kutokana na machafuko ya kisiasa.
Mshambuliaji huyu anatarajiwa kuiongoza Al Hilal kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ambao utachezwa kesho Novemba 26, 2024 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Yanga.
Abdel Rahman, anaaminika kuwa ataipa kazi ngumu safu ya ulinzi ya Yanga chini ya Dickson Job pamoja na Ibrahim Bacca ambao watakuwa wakimzuia asifunge, ikumbukwe kuwa nyota huyu aliwahi kuifunga Yanga mabao mawili, moja kwenye uwanja wa Mkapa na lingine alifunga Sudan msimu wa 2022/2023, wakati Yanga ilipotolewa na Al Hilal kwenye mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wanachotakiwa kufanya Job na Bacca
Safu ya ulinzi ya Yanga chini ya Dickson Job na Ibrahim Bacca wana kazi ngumu ya kumzuia Mohamed Abdel Rahman ambaye anaonekana kuwa mshambuliaji tishio wa Al Hilal.
Wamekuwa wakifanya kazi nzuri katika kuhakikisha lango lao linakuwa salama ambapo walifanya hivyo msimu uliopita kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns walipomzuia mshambuliaji hatari, Peter Shalulile ambaye akufanikiwa kupata bao kwenye mechi zote mbili.
Mchezaji mwingine ni Serhou Guirassy ambaye ni mshambuliaji wa Borussia Dortmund na timu ya Taifa ya Guinea ambaye alishindwa kufurukuta mbele ya Dickson Job na Ibrahim Bacca kwenye mchezo wa kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika (Afcon).
Yanga itakuwa nyumbani ikiikaribisha Al Hilal kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kesho Novemba 26, 2024 huku mara ya mwisho timu hizi zilikutana Oktoba 8, 2022 ambapo Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 kabla ya kwenda kupoteza ugenini bao 1-0 Oktoba 16, 2022.