Polisi Songwe yamalizana na Mdude, yamhamishia Mbeya

Songwe. Wakati Jeshi la Polisi mkoani hapa likimaliza mahojiano na Mdude Nyagali, mwanaharakati huyo amepelekwa tena mikononi mwa jeshi hilo mkoani Mbeya kwa mahojiano mengine, kujibu tuhuma zinazomkabili.

Nyagali alikamatwa Novemba 22, 2024 akiwa na makada wengine wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyansa, Joseph Mbilinyi, maarufu ‘Sugu’ mkoani Songwe kwa madai ya kukiuka taratibu za kampeni.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Novemba 25, 2024 Kamanda wa Polisi mkoani Songwe SACP, Agustino Senga amesema tayari wamemaliza mahojiano na mwanaharakati huyo na tayari ameelekea Mbeya kujibu tuhuma nyingine zinazomkabili.

Amesema Mdude alikuwa na kesi katika mambo matatu yaliyokuwa yanamkabili na kilichobaki ni mambo ya kitaalamu, hivyo kama itakuwa ni kupata dhamana itafahamika mkoani Mbeya.

“Sisi tumemaliza kumuhoji alikuwa na kesi tatu lakini hatujamuachia kwa kuwa upelelezi ni process (mchakato) kuna hadi mashahidi wengine ambao tutawatafuta kwa muda wao.”

“Alikuwa na wanasheria wake akaandika maelezo amepelekwa Mbeya ambapo huko alikuwa na kesi zake ikiwamo matamko, hivyo akikamilisha mambo ya dhamana yanaweza yakafanyika hapo,” amesema Kamanda huyo.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga kuelezea kushikiliwa kwa kada huyo wa Chadema amejibu kuwa yupo kikaoni akiomba kumrejea mwandishi baadaye.

Wakati huohuo, wakili Philip Mwakilima ameliambia Mwananchi tayari amefungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, akitaka kada huyo aachiwe huru au apelekwe mahakamani iwapo ana kesi ya kujibu.

Amesema wakati Polisi inaendelea kumshikilia, anaendelea na mchakato wa kufuatilia akieleza mtuhumiwa anapokamatwa anapaswa kuwa amechukuliwa maelezo ndani saa nne.

“Ni kweli nimefungua kesi jana na leo asubuhi imepokelewa nafuatilia kujua ni jaji yupi atasikiliza maombi hayo, mtu anapokamatwa ndani ya saa nne awe amechukuliwa maelezo na isitoshe nimezuiliwa kuonana naye,” amesema.

“Wamenithibitishia kwamba hawana mpango wa kumuachia bado wana kazi naye, ndiyo imenisukuma kufungua kesi tunachotaka ni aachiwe au aletwe mahakamani na Polisi ionywe,” amesema Mwakilima.

Related Posts