PAMOJA na kukiri matokeo kutokuwa mazuri, Kocha Mkuu wa KenGold, Omary Kapilima amesema bado ni mapema kuitabiria timu hiyo kushuka daraja badala yake wasubiri muda utaamua.
Mbali na hilo, pia ameeleza kuridhishwa na kiwango cha nyota wake namna wanavyobadilika katika kila mechi akieleza kuwa licha ya kuanza vibaya ligi, lakini wanaweza kumaliza kibabe, muhimu ni kutokata tamaa.
KenGold inayoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu kwa mara ya kwanza, haijawa na matokeo mazuri kwani katika michezo 12 iliyocheza imekusanya pointi sita na kuwa mkiani kwenye msimamo na kuweka presha ndani na nje ya uwanja katika kukwepa kushuka daraja.
Kapilima alisema pamoja na matokeo hayo, bado ni mapema kwa wadau na mashabiki kuikatia tamaa na kuitabiria kushuka daraja, akieleza kuwa lolote linawezekana.
Alisema wamekuwa na mwanzo mbaya lakini ligi haijaisha, wanao uwezo wa kupindua meza na kumaliza kibabe na timu ikabaki salama Ligi Kuu msimu ujao, akieleza kuwa wachezaji wanaonyesha ubora katika kila mechi.
“Ni sahihi matokeo si mazuri hadi sasa, lakini si kwamba ligi imeisha, tunaweza kuanza vibaya ila mwisho tukawa bora, hatuwezi kukata tamaa na wanaoitabiria mabaya wasubiri.
“Nachofurahishwa ni namna wachezaji wanavyopambana kila mechi, uliona mchezo dhidi ya Coastal Union tulitanguliwa lakini tukasawazisha huku tukiwazidi umiliki, naamini tutakuwa sawa,” alisema Kapilima.
Kuhusu maboresho kikosini dirisha dogo, alisema bado ni mapema badala yake muda utakapofika ataweka wazi kama atahitaji kuongeza au kupunguza kulingana na mahitaji ya timu.