Abrahaman kujipanga upya Mashujaa | Mwanaspoti

NYOTA wa Mashujaa, Abrahaman Mussa amesema msimu huu kwake umekuwa ni mgumu kutokana na ushindani wa namba katika kikosi hicho, japo ubora wa wachezaji wengine unamfanya kujituma zaidi uwanjani akipewa nafasi na benchi la ufundi.

Kauli ya nyota huyo imejiri baada ya kuifungia timu hiyo bao Novemba 23 mwaka huu katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Namungo, likiwa ni la kwanza kwake na kikosi hicho msimu huu, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

“Nimefurahi kufunga bao moja ambalo limesababisha kutupa pointi tatu katika mchezo ambao ulikuwa mgumu kutokana na kila upande kuhitaji ushindi, nimekosa michezo mitano kutokana na ushindani ila sijakata tamaa na nitapambana zaidi ya hapa,” alisema.

Nyota huyo mwenye uwezo wa kucheza beki na kiungo mshambuliaji, aliongeza kwamba anaheshimu wachezaji wenzake anaoshindana nao kwani ushindani siku zote ndio ambao huwasaidia kwa pamoja kutimiza malengo waliyojiwekea msimu huu, hivyo atapambana kadri ya uwezo wake wote kila atakapopewa nafasi hiyo.

Kwa upande wa Kocha wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ alisema ili timu ifanye vizuri ni lazima kuwepo na ushindani baina ya wachezaji wenyewe, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kutimiza malengo ya klabu tofauti na kutegemea mmojawao.

“Tunaposema ukubwa wa kikosi maana yake una wachezaji wazuri wawili au watatu kwa kila nafasi ambapo akikosekana mmoja wao huumizi kichwa, eneo langu la washambuliaji najivunia hilo na ni jukumu kwao kupambania nafasi ya kucheza,” alisema.

Abrahaman anakumbukwa zaidi msimu wa 2016-17, wakati akiwa na Ruvu Shooting ambapo alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 14, sawa na Simon Msuva aliyekuwa anaichezea Yanga japo kwa sasa anaichezea Al-Talaba SC ya Iraq.

Related Posts