Songwe. Serikali mkoani hapa kwa kushirikiana na wadau wa elimu, imezindua kampeni maalumu yenye lengo la kuandikisha na kuwarejesha shuleni watoto 11,043 waliokuwa nje ya mfumo wa elimu.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amebainisha hayo leo Jumatatu, Novemba 25, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Chongolo amesema kampeni hiyo ya miaka mitano inalenga kuondoa vikwazo vya kijamii na kifikra vinavyokwamisha watoto wengi kuendelea na masomo.
“Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya msingi ya elimu. Takwimu zinaonyesha bado kuna idadi kubwa ya watoto walio nje ya shule mkoani kwetu,” amesema Chongolo.
Aidha, amesema kampeni hiyo inalenga pia kuboresha miundombinu ya shule na kufanikisha lengo la uandikishaji wa asilimia 80 ifikapo mwaka 2025, kutoka asilimia 44 ya mwaka 2024.
Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, Mkoa wa Songwe umefanikiwa kuandikisha wanafunzi 4,826 wa mpango wa elimu ya msingi kwa waliokosa (Memkwa), wakiwemo wasichana 2,254 na wavulana 2,572. Zaidi ya hayo, wanafunzi 2,037 (wavulana 1,172 na wasichana 865) walirejeshwa kwenye mfumo rasmi wa elimu.
Chongolo ametoa wito kwa viongozi wa vijiji kuhakikisha watoto wote walioko nje ya shule wanatambuliwa na kurudishwa shuleni kama sehemu ya kufanikisha malengo ya kampeni hiyo.
Pia amezitaka kamati za shule kubaini changamoto zinazowakumba watoto na kuweka mikakati ya kuzitatua.
Aidha, amewataka viongozi wa halmashauri kusimamia uandikishaji wa watoto waliokuwa nje ya shule na kuhakikisha wanadhibiti mdondoko wa wanafunzi waliorejea shuleni.
Mathias Mwasenga akizungumza na Mwananchi Digital amesema mpango huo utasaidia kila mtoto kupata haki ya elimu.
“Mpango huu umekuja kwa muda mwafaka kwani watoto wengi waliacha shule kwa sababu ya ugumu wa maisha, hivyo ni muhimu kuwaunga mkono kwa kuwanunulia mahitaji ya shule,” amesema Mwasenga.