WAKATI taarifa zikisambaa kuwa Biashara United ipo sokoni, uongozi wa timu hiyo umekanusha, ukieleza kuwa wanachotafuta ni mdau atakayeweza kuongeza nguvu tu.
Hii ni baada ya aliyekuwa mdhamini wa timu hiyo msimu uliopita, Revocatus Rugumila kujiengua kikosini na kuiacha ikiwa na mwenendo usioridhisha katika Ligi ya Championship msimu huu.
Msimu uliopita timu hiyo ilikuwa na matokeo mazuri ikipewa nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara, lakini ikaishia katika hatua ya mchujo (playoff) ya kupanda daraja, ambako ilikwama katika dakika za mwisho.
Msimu huu hali imeonekana kuwa ngumu kwani katika mechi 10 ilizocheza hadi sasa imevuna pointi 10 na kuwa katika nafasi ya 11 huku hali ngumu ya kiuchumi ikitajwa kuiathiri zaidi ndani ya uwanja.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Agustino Mgendi aliliambia Mwanaspoti kuwa taarifa za kuuzwa si sahihi badala yake wanatafuta mdau atakayeweza kuwaongezea nguvu ili kuwa imara.
Alisema kinachowakwamisha kwa sasa kwenye ligi ni hali mbaya ya kiuchumi, hivyo yeyote anayetaka kuwekeza kikosini humo wanamkaribisha kwani ushirikiano na mazingira ni mazuri.
“Tunachotaka ni muwekezaji kama alivyokuwa Rugumila, hii ni mali na nembo ya wakazi wa Musoma, hatuwezi kuuza timu hii, kinachotusumbua kwa sasa ni hali ya uchumi,” alisema Mgendi.
Kiongozi huyo amekiri kuwa kwa sasa wanakabiliwa na madeni ya mishahara kwa wachezaji, huku akieleza kuwa matokeo yasiyoridhisha wanayopitia kwa sasa yatapita na timu itakuwa pazuri.