UTPC yazindua siku 16 za kupinga ukatili huku ikitahadharisha

Babati. Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), umezindua kampeni maalumu ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto mwaka 2024, kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Kauli mbiu ya kampeni hiyo inasema; ‘Baada ya miaka 30 ya Beijing Tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.’

Akizungumza leo Jumatatu, Novemba 25, 2024, katika uzinduzi uliofanyika mjini Babati mkoani Manyara, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Kenneth Simbaya amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kutokomeza ukatili.

Amehimiza waandishi washirikishwe kwa karibu katika mapambano hayo ili waweze kupata taarifa sahihi za kuhabarisha umma.

“Vyombo vya habari vina uwezo wa kushawishi fikra za watu, kwani watu huchukua muda kufikiria kwa kina baada ya kupata taarifa kuhusu vitendo vya ukatili kupitia vyombo hivyo,” amesema Simbaya.

Ameongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo, hivyo jamii,  viongozi wa taasisi na Serikali wanapaswa kushirikiana kwa karibu na waandishi.

“Hawa watu wanapoandika kuhusu changamoto pia huangazia mafanikio. Tanzania ya sasa imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita,” amesema Simbaya.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Elim Pentecoste Tanzania, Peter Konki amesema jamii ikielimishwa ipasavyo kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, itajiepusha na vitendo hivyo.

Pia amesisitiza kuwa Mkoa wa Manyara haupaswi kufurahia matukio mengi ya ukatili wa kijinsia, bali kuchukua hatua za kuachana nayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Manyara (MNRC), Zacharia Mtigandi amesema mkoa huo unashika nafasi ya pili kwa ukatili wa kijinsia kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021, huku ukiripoti matukio ya aina hiyo 3,400, ukitanguliwa na Mkoa wa Iringa.

Mtigandi amebainisha kuwa matukio mengi yanayoripotiwa mkoani humo ni ya vipigo, ubakaji na ukeketaji.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Manyara, Anna Fissoo amesema Manyara isiyo na ukatili inawezekana, lakini jamii inapaswa kuongeza juhudi za kupinga ukatili huo.

Amesisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa.

Related Posts