CRDB, Puma zaingia makubaliano kuimarisha usambazaji wa mafuta

Dar es Salaam.Katika jitihada za kuimarisha ujasiriamali na kukuza biashara nchini, Benki ya CRDB imeingia makubaliano na kampuni ya Puma Tanzania kuwakopesha wamiliki wake wa vituo vya mafuta nchini.

Makubaliano hayo yaliyosainiwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah yanatoa nafasi kwa wamiliki wa vituo vya mafuta vya Puma kukopa hadi Sh1 bilioni, ili kulipia mafuta wanayopewa na kampuni hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Nsekela amesema sekta ya nishati hasa mafuta nchini ndio uti wa mgongo wa uzalishaji mali, hivyo ni muhimu kwa wadau kushirikiana kwa ukaribu kuhakikisha Taifa linakuwa na mafuta ya kutosha wakati wote ili kufanikisha shughuli za uzalishaji mali ikiwamo uanzishaji viwandani, usafirishaji na uhifadhi.

“Leo tumekutana hapa kwa jambo moja kubwa la kusaini mkataba wa ushirikiano kati ya Benki ya CRDB, Puma Energy Tanzania pamoja na wafanyabiashara wanaoshirikiana nao katika kuimarisha biashara ya mafuta nchini. Kwa wafanyabiashara ambao wameshirikiana na Puma Energy walau kwa miezi sita, wanakidhi kupata mkopo wa mpaka Sh1 bilioni watakazozirejesha kwa miezi 12,” amesema Nsekela.

Uwezeshaji huu, Nsekela amesema unalenga kuondoa changamoto ya ukosefu wa fedha za kuagiza kiasi cha mzigo unaohitajika hivyo kuwanyima fursa za biashara wamiliki wa vituo pamoja na kampuni ya Puma Energy Tanzania.

Kwa kuitambua changamoto hiyo, Nsekela amesema Benki ya CRDB imekuja na ubunifu huo wa kuwawezesha wamiliki wa vituo vya mafuta, ili waweze kulipia kiasi chote cha mafuta wanachokihitaji na kuiwezesha Puma Energy Tanzania ambayo ni miongoni mwa waagizaji wakubwa wa mafuta nchini, kuingiza kiasi cha kutosha cha mafuta kwa ajili ya wateja wake.

“Kwa makubaliano haya, Benki ya CRDB itakuwa inatoa mikopo kwa wamiliki hawa wa vituo vya mafuta ili kulipia bidhaa wanazozihitaji kwa wakati, na kuifanya kampuni ya Puma Energy yenyewe kuwa na fedha za kutosha kuagiza mzigo mwingine kutoka nje. Tunaamini, utaratibu huu utarahisisha upatikanaji wa huduma zote zinazotakiwa vituoni hivyo kukuza biashara na sekta ya mafuta,” amesema Nsekela.

Kwa muundo uliopo nchini, waagizaji wakubwa wa mafuta hushindana katika zabuni zinazotangazwa na Wakala wa Ununuzi wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), kuingiza shehena ya mafuta kabla ya kuisambaza vituoni ili yauzwe kwa wananchi.

Mpaka Juni 30 mwaka huu, takwimu zinaonyesha kulikuwa na vituo 2,197 vya mafuta nchini.

 Nsekela amesema wakati mwingine vituo hivyo huhitaji mafuta mengi kuliko kiasi cha fedha walichonacho na kampuni kubwa kuwapa kadri iwezekanavyo.

“Utaratibu huu wa vituo kupewa mafuta kwa mkopo huzifanya kampuni hizi kubwa kukosa fedha ya kutosha zinapohitaji kuagiza mzigo mwingine kutoka nje na hapa ndipo  Benki ya CRDB inapoingia, ili kuweka mambo sawa na kukidhi mahitaji ya kila upande bila kuathiri mzunguko wa biashara,” amesema Nsekela.

Akieleza namna walivyojipanga kuwahudumia wafanyabiashara wa mafuta nchini, Nsekela amesema wana uzoefu wa kutosha kwani mpaka sasa, Benki ya CRDB imeshakopesha zaidi ya Sh134.4 bilioni katika sekta hiyo na ushirikiano waliouanza na Puma Energy Tanzania unakusudia kutanua zaidi wigo wa wanufaika.

Kwa upande wa Fatma amesema soko la mafuta nchini linakua kila siku na wao wanajitahidi kuleta bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wateja,  ili kusaidia kuchochea kukua kwa uchumi na maendeleo ya mwananchi mmojammoja.

“Malengo yetu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata bidhaa zenye ubora kwa ajili ya gari, mashine au mitambo yake anayoitumia katika uzalishaji.” Tunachokifanya sasa katika ushirikiano wetu huu na Benki ya CRDB ni kuhakikisha bidhaa zetu zinafika kila mahali tena kwa kiasi kinachohitajika, ndio maana wamiliki wa vituo wanapewa nafasi ya kuimarisha mitaji yao ya uendeshaji kwa kukopeshwa na taasisi hii kubwa zaidi ya fedha nchini,” amesema Fatma.

Kutokana na ushirikiano huu, Fatma amesema wanaamini wamiliki wa vituo vya mafuta wanaohudumiwa na Puma Energy Tanzania watakuwa na uhakika wa kupata bidhaa zote muhimu.

Related Posts