Beki mkongwe wa Simba, Shomari Kapombe amesema watatumia mchezo wa kesho kurudisha matumaini ya kutwaa taji msimu huu huku akikiri wananafasi kubwa ya kufanya hivyo.
Kapombe amesema benchi la ufundi limefanyia kazi maeneo yote lakini matatu ndio yalifanyiwa kazi kwa usahihi zaidi lengo likiwa ni kufikia malengo yao.
“Kocha ameangalia makosa kwenye mechi zilizopita amehakikisha mapunguvu eneo la kiungo, ukabaji na ushambuliaji yanakuwa imara zaidi ili kuhakikisha tunakuwa na mchezo bora na wa ushindani,” alisema na kuongeza;
“Mchezo uliopita tulipoteza kwa idadi kubwa ya mabao hatuwezi kurudia makosa pia naamini mchezo ujao utakuwa mzuri na wa ushindani malengo ni pointi tatu ili kurudisha mashabiki na tumaini la ubingwa,” alisema.
Kapombe alisema wao kama wachezaji wapo kwenye hali nzuri na kila mmoja anatambua umuhimu wa mchezo wa kesho na namna wanavyotamani kutwaa taji la ligi baada ya kukosa misimu miwili mfululizo.
Alisema wanaanza kwenye mchezo wa kesho ili kuweza kufikia lengo la kutwaa ubingwa huku akikiri ushindani ni mkubwa na kila timu inapambana kufikia malengo hayo.