Dar es Salaam. Wakati kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zikifikia kilele kesho, vyama vitatu vya CCM, Chadema na ACT Wazalendo vimeonyesha ushindani mkali kwenye maeneo vilivyosimamisha wagombea.
Kampeni hizo zimefanyika kwa siku saba kuanzia Novemba 20 hadi Novemba 26 ambapo viongozi wa vyama hivyo wamesambaa katika maeneo mbalimbali nchini, wakiwanadi wagombea wao kwa wananchi.
Licha ya vyama hivyo kuwa na hamasa kubwa katika uchaguzi huo, vyama vidogo pia vimefanya kampeni katika baadhi ya maeneo ambapo ama vimesimamisha wagombea au vinawaunga mkono wagombea wa vyama vingine.
Nafasi zinazogombewa kwenye uchaguzi huo ni pamoja na wenyeviti wa vijiji na mitaa na vitongoji pamoja na wajumbe ambapo CCM kimesimamisha wagombea katika nafasi zote 80,430, huku upinzani ukiweka kwenye nafasi 30,977 sawa na asilimia 38 ya nafasi zote.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), jumla ya Watanzania 31,282,331 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo, ambao ni sawa na asilimia 94.83 ya lengo la kuandikisha wapiga kura 32,987,579.
Licha ya kuwapo kwa malalamiko baada ya wagombea wao wengi kuenguliwa, viongozi wa vyama vya upinzani, kama ilivyo kwa wenzao wa CCM, wameendelea kufanya mikutano ya kampeni kwenye mitaa na vijiji wakihamasisha wananchi kuwachagua wagombea wao.
CCM inakimbizana dakika za mwisho za kampeni kwa kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali nchini, ambapoo viongozi waandamizi wa chama hicho wakionekana kutawanyika maeneo tofauti wakiwanadi wagombea wao.
Katika kuhitimisha kampeni hizo leo, chama hicho kitafunga kampeni zake za uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa namna ileile kilivyozindua kwa Katibu Mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi kuongoza uhitimishaji huo.
Dk Nchimbi anatarajiwa kuhitimisha kampeni za CCM mkoani Dar es Salaam katika uwanja wa Kwa Mnyani uliopo Wilaya ya Temeke.
Wakati huohuo, viongozi wengine, wakiwemo wajumbe wa kamati kuu na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC), watakuwa wakiongoza matukio kama hayo katika maeneo mengine nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Mongella atahitimisha kampeni Mkoa wa Shinyanga huku Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, akiongoza shughuli hiyo Mkoa wa Kagera.
Akihutubia wananchi wa Mwananyamala kwa Kopa, jana, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alisema chama hicho, kilizindua kampeni hizo Novemba 20,2024 kwa kishindo na kitafunga mchakato huo kwa kishindo kutokana na maandalizi mazuri.
“Huu, ndio mkutano wangu wa mwisho nakwenda Morogoro kufunga kampeni, nabadilishana na Katibu Mkuu (Dk Emmanuel Nchimbi), atakayefunga kampeni hizi Mbagala kesho (leo).
“Tumeamua kufanya mabadiliko haya ili kuleta hamasa, nawaomba wananchi kama mlivyojitokeza kwenye uandikishaji basi Jumatano mjitokeze hivyo hivyo kupiga kura,” alisema Makalla.
Wakati huohuo, viongozi wa Chadema nao wametawanyika katika kanda mbalimbali kukamilisha kampeni za chama chao dakika za lala salama kuelekea siku ya uchaguzi, kesho, Novemba 27.
Akizungumza na Mwananchi, jana, kuhusu mikutano yao ya mwisho ya kufunga kampeni, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe atafunga kampeni hizo Hai mkoani Kilimanjaro.
Mrema alisema Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu atakuwa na mkutano wa kufunga kampeni mkoani Singida wakati Katibu Mkuu, John Mrema akitarajiwa kuwa na mikutano mkoani Mtwara.
Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba Naibu Katibu Mkuu, Tanzania Bara, Benson Kigaila ataongoza ufungaji wa kampeni Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wakati Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu akiongoza shughuli hiyo Wilaya ya Tanganyika, Katavi.
Akizungumza kwenye mkutano wake, juzi, huko Kahama Shinyanga, Mwalimu aliwataka wakazi wa Kahama na Watanzania kwa ujumla kutodharau uchaguzi wa serikali za mitaa licha ya mchakato kuvurugwa.
“Tumeamua kushiriki katika uchaguzi huu sio kwamba ni shwari hapana, tumeona tushiriki ili hayo maeneo yatumike katika kupaza sauti zetu, hata kama wakimbakisha mmoja tutakusanyika Chadema wote kwenye hicho kijiji, mtaa au kitongoji,” alisema.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alisema chama chake kimejiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa na kwamba wana matumaini makubwa ya kushinda katika maeneo waliyosimamisha wagombea.
“ACT- Wazalendo tumejiandaa na huu uchaguzi tangu mwaka 2023 tulipozindua Brand Promise ya chama na kufanya mikutano ya hadhara.
“Vilevile, tuna ajenda kupitia ilani yetu tuliyozindua. Mwisho chama chetu tuna umoja na mshikamano wa dhati. Tunaenda kubadilisha sura ya nchi kisiasa. Tuna matumaini makubwa,” alisema Dorothy.
Mbali na Dorothy, kiongozi wa zamani wa chama hicho, Zitto Kabwe, naye anaendelea kuwanadi wagombea wa chama hicho kwa wananchi mkoani Kigoma kukamilisha kampeni za chama hicho mkoani humo.
Katika kuhitimisha kampeni za chama hicho leo, Zitto atakuwa Mtaa wa Kisangani, Uwanja wa Mwanga Center, Kigoma Mjini wakati Katibu Mkuu, Ado Shaibu akitarajiwa kufunga kampeni Tunduru mkoani Ruvuma.
Vilevile, Kiongozi wa Chama, Dorothy na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Bara, Issihaka Mchinjita watafunga kampeni Lindi mjini. Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Esther Thomas atakuwa Nyamagana mkoani Mwanza wakati mwenyekiti mstaafu, Juma Duni Haji akitarajiwa kuwa Dar es Salaam.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo alisema kwa siasa za Tanzania, vyama vya CCM, ACT Wazalendo na Chadema ndio vyama vikuu kwa sasa kwa namna vinavyojipanga na kutekeleza shughuli za kisiasa.
“ACT na Chadema vinafanya kazi sehemu kubwa ya Tanzania, tofauti na vyama vingine vya upinzani ndio maana kuna dhana kwamba vyama fulani vinatumika kuwezesha chama fulani.
“Vyama vya ACT, Chadema na CCM ndivyo vyenye uwezo kufanya mikutano mikuu na wanachama au watu wakaifuatilia na kuisikiliza kwa ukaribu,” alisema Dk Masabo.
Kwa mujibu wa Dk Masabo, ushindani kwa sasa upo vyama vya CCM, Chadema na ACT na endapo uchaguzi wa mwaka 2025 utaendeshwa kwa uhuru na haki hali hiyo itaongezeka zaidi.
“Kwa ushindani huu, ACT na Chadema wanatakiwa kukubaliana ili kuachiana baadhi ya maeneo ili kupata wabunge na madiwani wengi, wasipofanya hivyo kura watazigawa na CCM itashinda.
“Mahali popote ambapo kuna ACT na Chadema wasipokubaliana kura zao watazigawa, lakini za CCM haziwezi kugawanyika,” alisema Dk Masabo.
Mchambuzi mwingine wa siasa, Rainery Songea anasema vyama 16 vilivyobaki havina mafungu ya fedha ya kutosha yatakayowawezesha kufanya shughuli za kisiasa hasa kampeni za kuwanadi wagombea.
“Tuna vyama vingine ambavyo kujiendesha kwake kugumu, kuna vingine wanadai vyama vya mfuko, kuna vingine kodi za majengo vinadaiwa, sasa kama vinashindwa kulipa kodi vitaweza kufanya kampeni?
“Kwa mtazamo wangu hivi vyama vyote tungeviondoa tungebaki na vitatu au vinne ili kuwepo na ushindani, ukiangalia hivi vyama vidogo vinakwenda kugawana kura ambazo kiuhalisia zingemsaidia mgombea fulani,” alisema Songea.
Songea alisema CCM ina nguvu kubwa ikiwemo ruzuku, Chadema wana mtandao mkubwa wa wanachama wanaokichangia wakati ACT inaunda Serikali Zanzibar, inapokea ruzuku na ina wanachama pia katika maeneo mbalimbali.
“Ushindani wa ACT, CCM na Chadema unatoa changamoto na ukiona sehemu vipo basi vina nguvu, kitendo cha kumkamata Mbowe na mwenyekiti wa ACT kule Songwe maana yake wana nguvu, huwezi kusikia mwenyekiti wa chama cha UDP amekamatwa kwa sababu hana nguvu,’’ alisema Songea.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Aviti Mushi alisema uwepo wa ushindani wa vyama vitatu hauna afya sana huku akihoji vingine 16 vipo wapi kwa sababu vina usajili wa kudumu katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Upepo huu ndio utakaotueleza mchuano wa mwakani utakuaje, huku kwenye mitaa CCM ikichuana na upinzani, basi mwakani hali itakuwa hivyo.
“Ushindani unatusaidia wananchi kupata au kuchambua sera nzuri za vyama hivi ambapo kwa kipindi fulani vilikuwa kimya baada Serikali kufungia mikutano ya hadhara,” alisema Dk Mushi.