Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, Gervas Mgonja, kwa madai ya kutoa kauli za kuhamasisha wananchi kuvamia makazi ya wasimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku huu, Novemba 25 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, mtuhumiwa huyo amekamatwa baada ya kuonekana kwenye video mjongeo iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, akiwa anawahamasisha wananchi kufanya uhalifu Novemba 27,2024.
“Maneno hayo ya kuhamasisha vurugu, aliyatamka hadharani Novemba 24,2024, na baada ya kutamka waliyasambaza katika mitandao ya kijamii” amesema Kamanda Maigwa.
Aidha, amesema mtuhumiwa anachukuliwa maelezo ili hatua zingine za kisheria ziweze kufuata.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linatoa onyo kwa yeyote atakayethubutu kufanya vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjifu wa amani kabla,wakati na baada ya uchaguzi, hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila kumuonea muhali”amesema Kamanda Maigwa.
Akizungumzia kukamatwa kwa mwenyekiti huyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema amesema Mgonja ameshikiliwa kuanzia jioni ya leo.
“Ni kweli anashikiliwa na tuko naye hapa polisi, wanasema alitoa tamko lenye kuashiria kuvunja amani, alitoa tamko hilo Rombo Tarakea jana Novemba 24, kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi” amesema.
Ameongeza: “Limejadiliwa tunasubiri kuona linaishaje kwa sababu hatujaruhusiwa kuondoka, hivyo bado anashikiliwa na dhamana haijaruhusiwa”.