Tuanze tafakari ya leo na maneno ya busara ya Farrah Gray, Mmarekani mfanyabiashara maarufu, mwenye asili ya Afrika, aliyeandika: ‘’Jenga ndoto zako juu ya vipaji vyako, la sivyo mtu mwingine atakuajiri ili akutumie wewe kujenga ndoto zake.
Kwa maneno mengine ni kwamba mtu usipotumia vipaji vyako kujiendeleza mwenyewe, mtu mwingine atatumia hivyo vipaji vyako kwa maendeleo na faida yake mwenyewe.
Hii ni kama kusema: una shamba, hulitumii, lakini anakuja mtu anakuajiri ulime shamba hilo na faida yote anachukua yeye na kukulipa wewe mshahara kiduchu.
Au una gari la mizigo, hulitumii, anakuja mtu mwingine, wala si mjanja sana, anakuajiri uendeshe hilo gari kubeba mizigo yake, kisha anakulipa mshahara kidogo.
Mifano hii inaonekana ni kichekesho, lakini kiuhalisia, ndivyo ilivyo kwa mtu asiyetumia vipaji vyake kisha mtu mwingine anatumia hivyo vipaji vyako kwa masilahi yake binafsi.
Mwaka 1986 nilikamilisha utafiti ulioonyesha kwamba kila mtu ni tofauti na wengine. Hakuna pacha katika vipaji tulivyopewa na Mungu.
Watoto wawili pacha wana tofauti zao za kimaumbile na wazazi wao watakuhakikishia hilo.
Utafiti huo katika somo la falsafa ulionyesha kwamba tofauti ya mtu huyu na mtu yule ni kama DNA (Vinasaba vya urithi) ya damu yetu au alama ya vidole vyetu au muundo ya meno yetu.
Hivyo hoja ni kwamba kila mtu ana vipaji vyake vya asili ambavyo ni tofauti kwa kila mtu. Mwanafalsafa Martin Heidegger (1889-1976) anasema:
‘’ Si kwamba tu mtu ana vipaji, ukweli ni kwamba kila mtu ana vipaji visivyo na mipaka.’’
Ndiyo maana, utakuta mtu ni kiziwi, lakini shuhudia vinyago anavyotengeneza: hutaamini: ni vizuri ajabu.
Anthony de Mello (1931-1987) anatuambia hadithi ya binti mmoja huko India ambaye alikuwa wa kwanza kitaifa katika kucheza mitindo mbalimbali ya dansi (dancing artist).
Ikatokea akapata ajali na akapaswa kukatwa miguu yote miwili. Kila mtu akaamini kwamba huo ulikuwa mwisho wake wa kucheza densi.
Lakini si hivyo ilivyotokea. Alipata miguu bandia, akaanza kufanya mazoezi ya dansi na hiyo miguu bandia, mwishoni akafikia kilele cha mchezaji dansi bora katika taifa, huku akitumia miguu bandia.
Tafsiri yake: vipaji vyake havikuwa miguuni mwake, vilikuwa rohoni na akilini mwake.
Ninaamini kwa dhati kwamba kila mtu, na kila mtoto wetu na mwanafunzi yeyote yule, ana vipaji vyake ambavyo vinangoja kutumika kwa masilahi ya huyo mtu na kwa masilahi ya jamii yake.
Yaani kama mimi ni mwalimu wa chekechea, na nikapata wanafunzi 30 mwanzo wa mwaka wa shule Janauri 2025, nitakuwa na hakika isiyo shaka kwamba hapa darasani kuna vipaji vingi na vya ajabu ambavyo vinangoja kuibuliwa.
Nitatambua, bila ya shaka yoyote, kwamba hapa darasani kuna wanamuziki kama Michael Jackson, kuna wafanya biashara wakubwa, kuna maprofesa wa hali ya hatari.
Kuna wakulima watakaolisha nchi nzima, kuna wahandisi watakaojenga majengo ambayo hayataanguka kiholela.
Mwalimu bora ni lazima atambue hilo kila siku akiwa na wanafunzi wake. Mwalimu asiyetambua hilo asiruhusiwe kamwe kuingia darasani. Hatufai kabisa.
Sasa linakuja swali ambalo naulizwa mara nyingi na wasomaji wa makala zangu: nitatambuaje vipaji vyangu?
Nitatambuaje vipaji vya mwanangu? Nitatambuaje vipaji vya wanafunzi wangu? Hilo nimeulizwa mara nyingi.
Nitajaribu kujibu swali hilo lakini nakupa na wewe ujiongeze kwa kujitahidi kujibu swali lako mwenyewe, ukiongozwa na uzoefu wako wa maisha na shughuli unazozifanya sasa.
Napendekeza ujue haya mawili: kwanza: kila mtu ana vipaji, na ikitokea fursa ya kutumia kipaji fulani imekwisha, mtu huyo ataibua kipaji kingine.
Kwa mfano, mtu akiachishwa kazi ya ualimu kwa sababu yoyote ile, anaweza kuanza biashara fulani na akafanya vizuri sana.
Wakati anafanya biashara ya nguo, anaweza kuanza ufugaji wa kuku na akafanya vizuri sana. Ni kama vile kinyonga anavyoweza kujibadilisha rangi kulingana na mazingira yake.
Binadamu ana uwezo, huo, na hili shina shaka nalo kabisa, wa kujibadilishabadilisha kama kinyonga katika uwanja huu wa vipaji.
Pili: roho na akili ya mtu ni kama mpira unaovutika na ambao haukatiki. Hapa ndipo Heidegger anasema tuna vipaji bila mwisho, kwa Kiingereza: endless possibilities.
Utakuta huyu mtu ni fundi saa, nyumbani amefuga mbuzi wengi tu, yupo kwenye kwaya kanisani mwake, ni mweka hazina wa ukoo wake, ni mcheza karata hatari hapo kijijini mwake.
Bado yeye ni dereva wa tukutuku yake, na ikiharibika anajua kuitengeneza. Heidegger yuko sahihi: vipaji vyetu havina mipaka. Mwisho wa vipaji vya mtu ni pale anapoaga dunia hii.
Kwa hivyo nikizingatia haya mawili na mengine yaliyosemwa hapo juu, nitafanya yafuatayo kama mwalimu wa chekechea siku ya kwanza darasani.
Nitatumia siku ya kwanza kuwapa watoto nafasi ya kujitambulisha hata kama itachukua siku nzima au siku kadhaa.
Nitawapa nafasi watoto wajieleze kinagaubaga wazazi wao wanafanya nini na wao wanawasaidiaje wazazi wao.
Nitampa kila mtoto nafasi ya kusimama mbele ya darasa na kufanya chochote anachopenda mradi asivunje sheria za shule au asivunje heshima kwa yeyote.
Wakichoka darasani nitawapeleka nje ya darasa na kutembea nao bustanini kama shule ina bustani.
Nitakwenda nao uwanjani na kuwapa nafasi ya kucheza mchezo wowote wautakao. Wanaopenda kukimbia wakimbie, wanaopenda mpira wa miguu wafanye hivyo, na wanaotaka kitu kingine wafanye hivyo.
Lengo kuu hapa ni kuanza kutambua kila mtoto anapenda kufanya nini. Kwa siku nyingi nitafanya hivyo kama mwalimu.
Lakini kufanya hivyo kunahitaji mapinduzi ya fikara katika wizara ya elimu na katika fikra za viongozi wa siasa, wa dini na mashirika mengine.
Tuanze katika vyuo vya kutayarisha walimu. Somo kuu katika vyuo hivyo litafanana na makala hii ya leo.
Siku ya kwanza nikiingia darasani kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuwa walimu ningewataka waeleze kwa kinagaubaga kile kitu hasa wanachopenda kufanya.
Je, ni biashara, ni kulima, ni kufundisha? Nia ni kuwapa fursa ya kutambua kwamba wao wana vipaji vingi ili baadaye wawahamasishe wanafunzi wao kutambua hilo.