Mwisho wa mwaka umekaribia na shule zinatarajiwa kufungwa kwa mapumziko ya likizo ya mwaka.
Ingawa likizo ni wakati wa kupumzika, ni muhimu kuwa na ratiba inayojumuisha masomo, mazoezi, shughuli za kijamii, na muda wa kupumzika, ili kuhakikisha watoto wanakuwa na maendeleo bora katika nyanja zote za maisha.
Hapa nitaangazia baadhi ya mambo ambayo mzazi makini anapaswa kuyafanya msimu wa likizo.
Moja, kuendelea na programu ya kujisomea: Ingawa shule zitakuwa zimefungwa, mzazi unaweza kuchukua jukumu la kuhakikisha kwamba mtoto anabaki katika mrengo wa kimasomo, akijua fika likizo ni daraja la kurudi tena shule.
Sio wakati wa kumshurutisha kwa ratiba ngumu ya kujisomea kama anajiandaa na mitihani, ila mjenge kwa kumwekea ratiba ya kusoma kama njia ya kujikumbusha na kujiwinda na maisha ya shule mwakani.
Huu ndio wakati unaoweza kumhamasisha mtoto kusoma vitabu hasa vile vya fasihi na maendeleo ya utu.
Mzazi unaweza pia kuhamasisha watoto kutumia teknolojia kwa njia ya kujifunza kama vile kutumia programu za elimu na tovuti za kujifunza mtandaoni.
Mbili, weka ratiba ya mazoezi ya kimwili: Kipindi cha likizo kinaweza kuwa na hatari ya watoto kupunguza shughuli za kimwili, jambo ambalo linaweza kuathiri afya yao.
Wazazi wanapaswa kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata muda wa kutosha kwa mazoezi ya kimwili.
Hii inaweza kuwa kwa njia ya michezo ya nje, matembezi, au shughuli za kijamii zinazojumuisha mwili.
Mazoezi haya yatasaidia si tu katika kuboresha afya ya watoto, bali pia kuimarisha nidhamu na kujenga uhusiano mzuri kati ya wazazi na watoto.
Tatu, mfundishe ujuzi na stadi za maisha: Likizo ni fursa nzuri kwa wazazi kuwaelimisha watoto wao kuhusu maisha.
Huu ni wakati mzuri wa kuwafundisha watoto kuhusu majukumu ya kila siku kama vile kupika, kusafisha, au hata kuendesha baadhi ya shughuli za kifamilia.
Ujuzi huu utawasaidia watoto kuwa na ufanisi zaidi katika maisha yao ya kila siku na pia kuwaandaa kwa changamoto za baadaye maishani.
Nne, jenga uhusiano na familia: Kipindi cha likizo ni wakati mzuri wa kujenga na kuimarisha uhusiano wa kifamilia. Wazazi wanapaswa kutumia muda huu kwa ajili ya kufanya shughuli za pamoja na familia kama vile kupika pamoja, kutembelea maeneo ya burudani, au kushiriki katika shughuli za kijamii.
Tano, kuwahamasisha watoto kuwa na malengo: Wazazi wanapaswa kuchukua fursa hii kuwasaidia watoto wao kupanga malengo na kutengeneza mipango ya muda mrefu. Hii inaweza kujumuisha kujifunza masomo mapya au kuendeleza vipaji na talanta walizonazo.
Mwezeshe mtoto kuwa na malengo binafsi na namna ya kuyafikia.
Sita, muda wa kupumzika muhimu: Ingawa ni muhimu kuendelea na masomo na shughuli zingine, wazazi wanapaswa pia kuhakikisha watoto wanapata muda wa kupumzika na kufurahi.
Muache mtoto acheze, kutazama televisheni au kufurahia michezo ya kompyuta. Hii itamsaidia kurudi shuleni akiwa na nguvu mpya na motisha ya kujifunza.
Saba, tumia likizo kumpeleka mtoto kwa ndugu jamaa na marafiki. Hakuna kitu bora kama mtoto kujua nasaba yake.
Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kuwapeleka watoto kijijini kusalimia ndugu kwa wale wanaoishi mijini.