Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange amesema ujenzi wa barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka ya Kigogo – Tabata Dampo hadi Segerea ni miongoni mwa barabara ambazo zimepangwa kujengwa katika awamu ya tano ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Dugange ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Massaburi aliyehoji lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya mwendokasi inayotoka Kigogo – Tabata Dampo hadi Segerea.
Akijibu swali hilo, Dugange amesema awamu hiyo ya tano inajumuisha Barabara ya Nelson Mandela – (Ubungo hadi Daraja la Mwalimu Nyerere (Daraja la Kigamboni)) na Tabata – Segerea hadi Kigogo).
Amesema kwa sasa taratibu za kupata mkandarasi zinaendelea ambapo Mhandisi Mshauri atakayesimamia ujenzi ameshapatikana.
“Ninapenda kumhakikishia mheshimiwa mbunge kuwa fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni miongoni mwa barabara zitakazojengwa katika awamu ya tano zipo kupitia Washirika wa Maendeleo wa Ufaransa (AFD).
Aidha, akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbagala, Abdalah Chaurembo kwamba lini barabara ya mwendokasi ya Gerezani Mbagala itaanza kutumika, Dugange amesema barabara ipo katika hatua za mwisho hivyo hivi karibu itaanza kutumika.