Tanzania ilivyojiandaa kwa teknolojia ya Akili Mnemba kwenye elimu

Moshi. Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imejipanga kutoa mafunzo ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika vyuo vikuu hapa nchini, lengo ikiwa ni kuwapata watu ambao wataweza kuendana na teknolojia hiyo.

Alisema kwa sasa hakuna nchi duniani inayoweza kuthubutu kuacha kuwekeza katika teknolojia hiyo, na kwamba ikifanya hivyo itabaki nyuma sana kimaendeleo.

Mkenda aliyesema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Jubilei ya Mapadri wa shirika la kazi ya roho mtakatifu iliyofanyika katika Makao makuu yake Sabuko, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.

“Serikali inawekeza sana katika sayansi na teknolojia kwa sababu humo ndimo ambamo tunatengeneza hizi teknolojia za akili mnemba. Kwa mfano, sasa hivi tuna Samia Scholarship (Mfuko wa Udhamini wa Samia) ambayo wanapewa wanafunzi waliofaulu vizuri katika masomo ya sayansi kidato cha sita, ilimradi wawe wamesona hapa nchini katika maeneo ya Tehama hisabati, sayansi, uhandisi na elimu tiba,”alisema Profesa Mkenda.

Alisema kwenye hisabati na Tehama, hayo ni maeneo yanayomwandaa mtu zaidi katika kuendeleza vitu vyote hivyo vinavyoundwa na teknolojia ya Akili Mnemba.

“Tuna tawi la Indian institute of technology limeanziahwa Zanzibar tayari kinachukua wanafunzi na wanafundishwa Teknolojia hiyo, na sisi humu katika vyuo vyetu vikuu tunaweka programu kama hizi kwa ajili hiyo,”alisema Profesa Mkenda na kuongeza:

“Kubwa zaidi ni kuwekeza sio kuweka tu program hii. Tunataka kuvuna watu ambao watakuwa na uwezo mkubwa sana wa kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo vinafanya kazi kana kwamba vina akili. Kwa hilo kwa kweli tunawekeza, hakuna nchi ambayo itathubutu kuacha kuwekeza kwa sababu tutabaki nyuma sana.”

Alisema tangu kuanza kwa mpango wa ufadhili wa Rais Samia, maarufu Samia Scholarship, wanafunzi wengi wanaofanya vizuri sasa wanasomea masomo ya sayansi, kitu aklichokieleza kama dalili njema.

Alisema zamani wanafunzi waliosoma masomo ya PCM (fizikia, kemia na hisabati) na kupata ufaulu wa A zote, walikuwa wakienda kusoma masomo ya biashara kwa ngazi ya elimu ya juu, lakini tangu kuanza kwa ufadhili huo wanafunzi hao wanapendeleo masomo ya sayansi.

Wakati huohuo, Profesa Mkenda alisema ifikapo mwaka 2027 elimu ya lazima nchini itakuwa ni miaka 10 badala ya miaka saba. “Sasa hivi ikifika 2027 elimu ya lazima Tanzania itafika ni miaka 10 badala ya miaka saba, tutaweka sheria na miundombinu kila sehemu,”alisema.

Aliongeza:” Sisi ndio nchi pekee tumebaki duniani ambapo elimu ya lazima ni miaka saba, mtoto anaanza shule akiwa na miaka sita anamaliza darasa la saba na miaka 13, halazimiki kuendelea na shule, akiondoka huko watu wanalamika mbona haajiriki.”

Alisema katika mageuzi hayo, baada ya wanafunzi kuhitimu darasa la sita, sekondari kutakuwa na mikondo miwili; mkondo wa jumla na ule wa elimu ya amali.

Related Posts