62 mbaroni kwa tuhuma za wizi, uhamiaji haramu Shinyanga

Shinyanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakamata watu 62 wakiwamo raia saba wa Burundi kwa kuingia nchini bila kibali huku 55 wakituhumiwa kuhusika na wizi wa vitu mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Novemba 26, 2024 na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Janeth Magomi wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema wahamiaji haramu watatu walikamatwa Novemba 13, 2024 Kijiji cha Mseki na Novemba 17, mwaka huu wahamiaji hao wengine wanne walikamatwa Kijiji cha Nyamilangano Wilaya ya Ushetu wote wakiwa raia wa Burundi.

“Wahamiaji hao waliokamatwa Wilaya ya Ushetu wote ni raia wa Burundi na wamepelekwa katika ofisi za uhamiaji kwa hatua zaidi,” amesema Magomi.

Amesema operesheni na misako ya kuwatafuta wahalifu imewezesha kukamatwa watu wengine wanne pamoja na gari aina ya fuso ikiwa imebeba mifuko ya mbegu za pamba 210 ikiwamo ya wizi bila kufuata utaratibu.

“Gari hili (fuso) lilibeba mifuko 210, kati ya hiyo mifuko 107 iliibwa Chama cha Msingi cha Amcoss Mwamishoni na Novemba 23, 2024 katika Kijiji cha Maganzo Wilaya ya Kishapu alikamatwa mtuhumiwa mmoja kwa kuuza mbegu za pamba za ruzuku ya Serikali gunia 30 kwa mtu ambaye bado anatafutwa,”amesema Magomi.

Katika hatua nyingine, amesema ndani ya mwezi mmoja kuanzia Oktoba 24 hadi Novemba 25, 2024 jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 51 (majina yamehifadhiwa) wakiwa na vitu mbalimbali ikiwamo bangi kilo 10, pikipiki tisa zinazozaniwa za wizi.

“Pombe ya moshi lita 15, godoro nne, kontena mbili za bati, mashine tatu za bonanza, gari aina ya fuso ikiwa na nondo 130, binding wire 11, mifuko ya saruji 100, gari aina ya Toyota Noah lililotumika kubeba vitu vya wizi ambavyo ni pamoja na simu mbili, redio saba, kabati moja, jokofu moja na kitanda kimoja cha mbao,”amesema Magomi.

Kamanda huyo amesema jeshi hilo limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara na vikundi vya ulinzi kuhusu kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa pamoja na ukamataji salama wa uhalifu.

“Pia, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi katika shughuli ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na pia litahakikisha usalama kwa wanachi wote watokapo majumbani kwao, wawapo kwenye vituo, wakati wa kupiga kura na wakati wa kurejea nyumbani,” amesema.

Related Posts