Dar es Salaam. Idadi ya vifo vilivyotokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa, Kariakoo jijini Dar es Salaam vimefikia 29, baada ya miili mingine tisa kupatikana.
Jengo hilo liliporomoka asubuhi ya Jumamosi Novemba 16, 2024 na kusababisha vifo, majeruhi zaidi ya 80 na uharibifu wa mali za mamilioni ya fedha.
Leo Jumanne, Novemba 26, 2024, Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba akizungumza na waandishi wa habari akiwa eneo hilo la jengo lilipoporomoka amesema miili hiyo tisa imepatikana wakati shughuli ya kuondoa kifusi ikiendelea.
Makoba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo amesema shughuli ya uokozi imefikia tamati leo Jumanne Novemba 26.
Majengo mawili yachunguzwa
Majengo mawili yaliyopo pembezoni mwa ghorofa lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi, yanaendelea kuchunguzwa, imeelezwa.
Wakati uchunguzi ukiendelea kwa majengo hayo, mengine yameruhusiwa kufunguliwa kuanzia saa nane mchana wa leo Novemba 26, 2024.
Jengo hilo la ghorofa nne lililoporomoka Novemba 16, 2024 limesababisha vifo vya watu 29 na wengine 88 kuokolewa.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Thobias Makoba akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 26 amesema baada ya kuhitimisha shughuli ya uokozi maduka yaliyokuwa yamefungwa yanaruhusiwa kuendelea na biashara.
Kuhusu usalama wa majengo mawili ya ghorofa yaliyo pembezoni mwa lililoporomoka, ambalo moja lilitumika kama njia ya kuwafikia watu walionasa, Makoba amesema yote yatachunguzwa na wataalamu na kujiridhisha kuhusu usalama wake.
Endelea kufuatilia Mwananchi.