Mgombea Chadema adaiwa kutekwa, Polisi yaanza ufuatiliaji

Mwanza. Ikiwa imebaki siku moja kufanyika uchaguzi wa Serikali za mitaa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kuwa mgombea wake katika nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa wa Buswelu ‘A’ wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Pastory Apolinary ametekwa.

Madai ya kutekwa kwa mgombea huyo yametolewa leo Jumanne Novemba 26, 2024, na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za kanda zilizopo Nyegezi jijini Mwanza.

Wenje amedai ofisi yake ilipokea taarifa ya mgombea huyo kutekwa jana Novemba 25, 2024, saa saba mchana baada ya kukamilisha maandalizi ya eneo ulipotakiwa kufanyika mkutano wake wa hadhara.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje

Hata hivyo, akizungumza kwa simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema anaanza kufuatilia madai hayo ya kutekwa ili kubaini ukweli.

Akizungumza na wanahabari Wenje amesema: “Ilipofika mida ya saa saba (jana) akapata simu mtu akampigia akamwambia mimi ni mdau wa Chadema nataka niwape mchango kidogo kwenye kampeni kwa hiyo kwenye mida ya saa saba mchana alienda nyumbani kwake kuacha mizigo kisha akaenda kuonana na huyo mtu ndivyo amepotea hatujawahi kumuona tena tangu hiyo jana.”

“Tumeenda kwenye familia yake na wao hawana taarifa hawajui alipo simu zake hazipatikani. Usiku viongozi wetu walienda kutoa taarifa polisi na asubuhi hii (leo) Mwenyekiti wa Mkoa wa Chadema ameenda kuonana na RPC ili tujue way forwad (hatua inyofuata) watusaidie kutrack kujua nani alimpigia simu mara ya mwisho,” amesema Wenje.

Kutokana na uwepo wa tukio hilo, Wenje amesema mwenendo wa uchaguzi huo ni mgumu huku akidai utakuwa na mambo mengi na kusisitiza kuwa Chadema inaamini mgombea huyo ametekwa.

“Hali ni ngumu na huu uchaguzi una mambo mengi, kwa hiyo mpaka sasa mgombea ambaye tunaamini ametekwa kwa sababu tu ananguvu katika mtaa anaotoka wa Buswelu ‘A’. Naomba Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza wafanye jitihada za kupatikana mtu huyu akiwa hai,” amesema.

Akizungumzia hilo, kamanda Mutafungwa amekanusha kuwa na taarifa ya mgombea huyo kutekwa huku akisema anaanza kulifuatilia ili kubaini ukweli wa madai ya mwanasiasa huyo kutekwa.

“Mimi kwanza ndiyo kwanza nalisikia hilo tukio na sijaongea na kiongozi yeyote siyo wa Chadema, kiongozi yeyote wa chama cha siasa labda uwashauri tu mimi nipo sasahivi napatikana Mabatini hapa lakini kusema kwamba wameonana na mimi hapana,” amesema kamanda Mutafungwa.

 “Nimeshinda ofisini kwa mkuu wa mkoa sijakutana na kiongozi yeyote wa chama chochote zaidi ya askari wangu, washauri tu mimi niko hapa Mabatini waje wanione na hizo taarifa ngoja nizifuatilie.”

Katika hatua nyingine, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obad amewataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwawezesha wagombea wao kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini unatarajiwa kufanyika kesho Jumatano Novemba 27, 2024 nchi nzima.

Related Posts