Songea. Mkuu wa Programu wa Wizara ya Afya, Dk Catherine Joachim amesema takwimu zinaonesha Mkoa wa Ruvuma ni kinara katika upimaji wa Virusi vya Ukimwi (VVU), kwa asilimia 79, huku ukifanya vema katika kutekeleza malengo ya 95 tatu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Ruvuma inaongoza ikifuatiwa na Mkoa wa Njombe kwa asilimia 78.2 na Shinyanga kwa asilimia 78.
Malengo hayo yanaakisi asilimia 95 ya Waviu wawe wametambua hali zao, asilimia 95 wawe wamewekwa katika huduma ya tiba na asilimia 95 ya walio kwenye tiba wawe wamefanikiwa kufubaza VVU ifikapo mwaka 2025.
Hayo yameelezwa Novemba 25, 2024 na Dk Catherine alipozungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, ambayo kwa mwaka huu yataadhimishwa mjini Songea Desemba mosi.
Amesema kutokana na mwamko wa upimaji, hali ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi katika Mkoa wa Ruvuma, imepungua kwa asilimia 0.7 ikiwa ndiyo mkoa unaoongoza nchini.
Katika mkoa huo, maambukizi yameshuka kutoka asilimia 5.6 mwaka 2016/17 hadi asilimia 4.9 mwaka 2022.
“Kilichojificha nyuma ya kupungua kwa maambukizi katika mkoa huu, wananchi wake wamekuwa wakipima mara kwa mara kujua afya zao,” amesema Dk Catherine.
Pia, amesema asilimia 99 ya wanaotumia dawa za kufubaza makali ya VVU, tayari wameshafubaza virusi jambo linaloonesha Ruvuma imepiga hatua ikilinganishwa na mwaka 2016/17.
“Japokuwa mkoa upo nyuma ukilinganisha na wastani wa kitaifa wa 95/95/95 lakini 95 ya kwanza kitaifa tupo asilimia 83, 95 ya pili tupo asilimia 98 na 95 ya tatu tupo asilimia 94,” amesema Dk Catherine.
Ameeleza kutokana na Mkoa wa Ruvuma kuendelea kukua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo, migodi ya makaa ya mawe na madini mengine, usafirishaji na uvuvi maendeleo hayo yameleta nakisi kubwa kwenye usawa unaosababisha baadhi ya makundi kuwa katika hatari zaidi ya maambukizi ya VVU.
Aidha amesema kuwa, uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa vijana wa kike kati ya miaka 15 na 24 wameendelea kuwa katika hatari hasa katika miji na vitongoji yanakopita malori yakusafirisha makaa ya mawe, kwenye machimbo madogo madogo na kwenye shughuli za uvuvi.
Awali, akizindua maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema wanaoishi na VVU mkoani humo ni 68,237.
“Ndugu viongozi pamoja na wananchi halmashauri zetu zinazoongoza ni Manispaa ya Songea ikifuatiwa na Tunduru lakini vile vile na Halmashauri ya Mbinga, hivyo napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote kuzingatia tiba na matunzo, vilevile kuendelea kutumia dawa za kufubaza kwa kuwa hiyo njia pekee ya kuendelea kupambana na matatizo haya,” amesema.
Mwakilishi wa Baraza la Watu wanaoishi na VVU na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Nacopha, Letisia Moris amesema hali ya unyanyapaa na ubaguzi ni changamoto.
“Niwaombe viongozi wa dini, viongozi wa kimila na Serikali kwa nafasi zao kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya udhalilishaji ,unyanyapaa na ukatili kwa watu wanaoishi na VVU kwa kufanya hivi tutakuwa na jamii iliyostaraabika na yenye uwelewa mkubwa wa namna ya kuheshimu haki za binadamu,” amesema.