Unguja. Licha ya kuwa na kituo cha afya kilichojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wajawazito wa visiwa vya Uzi na Ng’ambwa Mkoa wa Kusini Unguja, wanaendelea kusotea huduma za uzazi kutokana na ukosefu wa madaktari na wauguzi kwa takribani mwaka mmoja sasa.
Ng’ambwa ina wakazi 1,158 kati ya hao wanawake ni 571 na wanaume 587, huku Uzi ikiwa na wakazi 3,075 kati ya hao wanawake ni 1,510 na wanaume 1,565. Wote wanategemea kituo hicho cha afya kilichopo Kisiwa cha Uzi kwa ajili ya huduma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Ahmed Suleiman Abdulla aliahidi siku ya ufunguzi wa kituo hicho wakati wa shamrashamra za Mapinduzi Desemba 27, 2023 kuwa kitapelekewa wataalamu wa afya.
Daktari dhamana (mganga mfawidhi) wa kituo hicho cha afya, Saleh Lilah Ali akizungumza na Mwananchi Novemba 25, 2024 ameeleza ugumu wanaokumbana nao katika utoaji huduma, akikiri kuwapo uchache wa wafanyakazi kwamba kuna muuguzi mmoja na daktari mmoja ambaye ni yeye.
Daktari huyo pamoja na muuguzi hawaishi kwenye visiwa hivyo, bali huenda kutoa huduma na kuondoka.
“Changamoto ni nyingi tunajua wanawake wapo na wanajifungua nyumbani, hawezi kuja hapa kwa sababu ya uchache wa wafanyakazi na hatuwezi kutoa huduma saa 24 kwa sababu ya uchache huohuo,” amesema Dk Saleh akiiomba Serikali iongeze wafanyakazi.
Amesema kwa mwezi mmoja wanafikisha wastani watu 300 hadi 500 wanaopatiwa huduma katika kituo hicho.
Kwa upande wa watoto, amesema wanafika takribani 100, huku wajawazito wanaohudumiwa wakikadiriwa kufikia 60 kwa mwezi.
Ili kutoa huduma nzuri kulingana na wananchi wanaohitaji huduma katika kituo hicho, Dk Saleh amesema angalau kwa uchache wanahitajika wauguzi watano na madaktari watatu.
Kwa mujibu wa miongozo ya Shirika la Afya Dunia (WHO), muuguzi mmoja anatakiwa ahudumie wajawazito wasiozidi watano.
Dk Saleh amesema wanawaelekeza wajawazito wanaofika wakati wa kujifungua, waondoke kisiwani humo kutafuta sehemu ya kuishi karibu na hospitali ambako watapata huduma zote kwa usalama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanawake wakazi wa visiwa hivyo wamesema wanapata huduma za kujifungua Kitogani au Unguja Ukuu lakini wanakumbana na kikwazo cha barabara kwani kuna daraja ambalo halipitiki muda wote kutokana na maji kujaa na kuondoka kulingana na mfumo wa bahari.
Asha Said Ali, mkazi wa Uzi amesema: “Tunapata matatizo kila kukicha, mwanangu hivi majuzi alikuwa mjamzito, alipata uchungu nikaja naye hapa nikaambiwa niondoke naye twende Unguja Ukuu, nilipofika huko nikaambiwa nimpeleke Kitogani.
“Hapo nilisikia akili yangu kuchanganyikiwa, na uchungu tunaujua sote kina mama jinsi unavyouma, inakuwa tafrani tupu,” amesema.
Ashura Said, amesema: “Kutokana na hali hii, nimeshawazalisha wanawake watano wakiwa nyumbani kwa nyakati tofauti, hiyo ni hatari lakini ndiyo hivyo tunamuomba Mungu. Utafanyaje, inabidi ufanye hivyo kwa kubahatisha tukizidi kumuomba Mungu alete usalama.”
“Nimewahi kumzalisha mama mmoja kwenye gari wakati tunampeleka Unguja Ukuu, tulipofika kwenye daraja tukakuta maji yameshajaa, hatukuwahi kuvuka, kwa hiyo akajifungua kwenye gari lakini tunashukuru Mungu alijifungua salama,” amesema.
Hajiram Ramadhan Aidar, amesema kujifungulia nyumbani unapoteza damu nyingi na kuongeza: “Sasa hapo kuna mawili, kupoteza maisha au kunusurika.”
Mwinzuma Arah Khamis kutoka Shehia ya Ng’ambwa, naye amesema ameshawahi kuwasaidia wajawazito kujifungua.
“Kwa sisi wanawake wa huku ni changamoto kubwa, ukifika wakati wa kujifungua unaambiwa nenda mjini ili siku ya kujifungua uwe salama, lakini kama una watoto wengine roho yako inakuwa ngumu kukaa huko huku nyumbani hujui watoto wako wanaishije. Ndiyo maana unabahatisha unasubiri uchungu uje ndipo uondoke au wakati mwingine watu wanaamua kuzalia nyumbani,” amesema.
Wanaeleza kutokana na vipato vyao, wanapata changamoto kugharimia nauli za kufuata huduma ng’ambo.
“Ukichukua bodaboda, watu wawili mnalipa Sh8, 000 kama ni boti mnalipa Sh10, 000, lakini mjamzito kumpandisha kwenye pikipiki na njia yenyewe ilivyo mbovu unamwongezea uchungu mara mbili,” amesema Mwinzuma.
Mashavu Mabrouk Khamis, amesema kwa kuwa kuna tatizo la uhaba wa madaktari na wauguzi, Serikali iwaruhusu wakunga wazalishe lakini iwapatie mafunzo angalau ya miezi mitatu ili wapate ujuzi.
Amesema wakati wa kufungua kituo hicho waliahidiwa kupewa wataalamu wote lakini wanasikitika kuona ahadi haijatekelezwa.
Maliki Mbaraka Makame, amesema wataalamu wawili waliopo hawaishi katika kisiwa hicho bali hufika na kuondoka ilhali kuna nyumba kwa ajili yao.
“Sijaona mpaka sasa madaktari wakikaa hapa, wanakuja na kuondoka hatujui kwa nini inakuwa hivyo. Serikali inatakiwa iwaajiri wazawa wa hapa kijijini, hili litapunguza adha hii ya wataalamu kutokaa hapa,” amesema.
Ahmed Ali Mussa, mkazi wa Shehia ya Ng’ambwa amesema baadhi ya wanawake hawana ndugu nje ya kisiwa hicho, hivyo hushindwa kuondoka wakati wa kujifungua.
Shekha wa Shehia ya Uzi, Othman Mwinyi Haji amesema changamoto hiyo imekuwa ya muda mrefu licha ya kujengewa kituo hicho kipya bado kilio ni kilekile.
Amesema tangu kituo hicho kifunguliwe mpaka sasa ni mwaka mmoja lakini huduma zinazorota wakati mwingine wataalamu hao wanashindwa kufika kwa sababu ya maji kujaa kwenye daraja.
“Akikuta maji yamejaa anasubiri mpaka yatoke, kama yamejaa saa mbili asubuhi basi mpaka yatoke inakuwa saa nane mchana, kwa hiyo hawezi tena kuja, huku kwanza hata muda wenyewe wa kufunga kituo unakuwa umeshafika,” amesema.
Othman amesema: “Hivi karibuni mjamzito alijifungua akiwa kwenye fiber (boti) anapelekwa Unguja Ukuu, hata yule nahodha alipoona mwanamke huyo kazidiwa akaanza kujifungua, alichumpa (kuruka) ili kuwaachia wanawake wamshughulikie.”
Ameiomba Serikali iwapatie wauguzi na madaktari ambao watahudumia wananchi kwa saa 24, akieleza kituo hicho pamoja na changamoto zilizopo kinafungwa saa 9.00 alasiri.
Amesema suala la wajawazito kulazimika kwenda kwa ndugu wanapofika hatua ya kujifungua inawapa kero.
“Kuna ndugu hawapendi kukaa na watu ila mtu anamkubalia kwa sababu ya muhali tu ila kiuhalisia inakosesha amani,” amesema.
Amesema iwapo kungekuwa na njia nzuri ingewasaidia hata inapotokea dharura kuwahi kwenda ngambo katika vituo vya afya vingine.
Akizungumzia hali hiyo, Daktari Dhamana (Mganga Mkuu) wa Wilaya ya Kati Unguja, Dk Amina Hussein Pandu amesema Serikali inajipanga kuwezesha ktuo hicho kutoa huduma.
“Kitu kimoja kikubwa cha kufanya ni kuwa na gari na boti ya dharura na itafutiwe sehemu ya kukaa, hivyo ndiyo vitu wizara inajipanga navyo,” amesema.
Amesema vituo vina madaraja na hicho bado kipo katika daraja la kwanza ila kikifika la pili kitaweza kutoa huduma zote.
“Serikali inajipanga, tunaomba wawe wastahimilivu waipe muda, bado inaweka mazingira kwa kina mama. Kwa sasa kinachotakiwa angalau kuwa na boti na gari la dharura ili mama akipata uzazi pingamizi aweze kusafirishwa,” amesema.
Dk Amina amesema kituo hicho hakina uhaba wa watumishi kwa kuwa wameshapelekwa. Hata hivyo, hakuwa na jibu la moja kwa moja la idadi ya waliopelekwa na jumla ya wataalamu waliopo katika kituo hicho kwa sasa.
Kuhusu wataalamu hao kukaa kisiwani humo, amesema hawana amri ya kumlazimisha kukaa kwenye nyumba hizo kwa sababu wengine wanafamilia zao nje ya Uzi.
Kuhusu wakunga kuruhusiwa kuzalisha, Dk Amina amesema: “Wakunga wa wajadi kwa sasa tunawaomba wawapeleke wajawazito kituo cha afya ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.”
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Khalid Mohamed Salum amesema tayari Serikali ipo kwenye mchakato wa kuweka miundombinu ya barabara na ujenzi wa daraja katika eneo hilo.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 8.72 na daraja likiwa na urefu wa kilomita mbili na upana wa mita 6.5 litaweza kupitisha magari mawili kwa pamoja.
Pia kutakuwa na njia ya waenda kwa miguu na reli za kuzuia ajali. Daraja hilo amesema litakuwa na urefu wa mita nne na nusu kwenda juu.
Amesema Sh35 bilioni zitatumika katika ujenzi wa barabara na daraja hilo, hivyo kuondoa changamoto hiyo ya muda mrefu.