ZOEZI LA UOKOAJI KARIAKOO LAHITIMISHWA, WAFANYABIASHARA WARUHUSIWA KUFUNGUA BIASHARA ZAO

MSEMAJI Mkuu wa serikali Thobias Makoba amesema kuwa zoezi la uokoajiKariakoo limefikia hatua ya mwisho hii leo Novemba 26, 2024 na shughuli nyingine kuanza kama kawaida kuanzia muda wa saa nane Mchana.

Aidha Msemaji huyo amethibitisha kuwa Serikali na Mamlaka nyingine za biashara zitashirikiana kwa kukaa pamoja na wafanya biashara na wakazi wa eneo hilo ili kuweka utaratibu wa kurejea kwa hali ilivyokuwa hapo awali.

Hayo ameyasema leo Novemba 26, 2024 jijini Dar es Salaam alipofika na kujiridhisha hali iliyopo katika eneo la jengo lililokuwa limedondoka huku akieleza kuwa Vifo vya watu waliofariki dunia katika jengo hilo ikifikia 29.

Makoba, ameeleza kuwa idadi ya vifo vilivyotokana na kuporomoka kwa ghorofa hilo pia zoezi linaloendelea la kutambua miili mingine kwa kutumia teknolojia ya vinasaba(DNA) na wakishathibitisha watatoa taarifa.

Akizungumza katika eneo la jengo lililoporomoka, Makoba amesema “Mpaka kufikia muda huu ambao tunazungumza kwa bahati mbaya namba ya marehemu ambao tumethibitisha ni 29, kwahiyo namba imeongezeka kidogo tunaendelea kuwaombea wenzetu wapumzike kwa amani.”

“Lipo zoezi linaloendelea la kutambua miili mingine kutumia teknolojia ya vinasaba(DNA) na wenyewe tutatoa taarifa tukishathibitisha Ndugu pamoja na miili ya wenzetu, kwa upande wa majeruhi idadi ipo palepale.” Ameeleza Makoba.

Related Posts