Viongozi wa vyama vya siasa wametumia siku ya leo kunadi sera za vyama vyao, kutoa elimu ya mpiga kura huku wakilia rafu dhidi ya mchakato wa uchaguzi na wagombea wao.
Soma: Kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zaanza Tanzania
Msemaji wa ACT Wazalendo anayehusika na masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Rahma Mwita amelaani vikali matukio ya kutekwa, kukamatwa, na kutishiwa kwa viongozi wa chama hicho saa chache kabla ya uchaguzi.
“Tulisema kama wapinzani na tulisema kama chama, msimamo weru ni kwamba hatuwezi kujiengua, kwamba tutapambana mpaka dakika ya mwisho. Lakini changamoto ni kwamba kila kikiondoka kikwazo hiki kinakuja kingine. Hatuwezi kukubali hili jambo. Kama tumeamua kufuata demokrasia ya vyama vingi, tufuate demokrasia.”
Mkurugenzi wa Itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa CHADEMA, John Mrema amesema chama chao kimefanikiwa kufanya kampeni nchi nzima na lakini wakatoa angalizo kwa serikali.
“Tuseme tu kwamba kwa sasa tunapokwenda kumaliza kampeni hizi, tunatoa wito kwa serikali, kuhakikisha kwamba haya tunayoyasikia hayatavuruga uchaguzi kesho.”
Kwa upande wa CCM, wao wameendeleza kampeni zao ambapo Katibu Mkuu wa chama hicho Emmanuel Nchimbi leo amehitimisha kampeni hizo jijini hapa, eneo la Mbagala, jimbo la Temeke.Upinzani Tanzania walalamika wagombea uchaguzi wa serikali za mitaa kuenguliwa kiholela
Wakati huo huo, Jeshi la polisi katika taarifa yake iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime imeeleza kuwa atakayesababisha uvunjifu wa amani,kesho, hataonewa muhali bali atachukuliwa hatua za kisheria.
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(ORTAMISEMI) imetoa mambo 9 ya kuyazingatia kesho wakati wa kupiga kura na kuwataka wananchi kuondoka eneo la kupiga kura mara baada ya kumaliza zoezi hilo.Tanzania: yasema wagombea wa upinzani wanaweza kukata rufaa
Uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kesho Novemba 27 kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Utajumuisha uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, kata, vitongoji na vijiji kwa Tanzania nzima.