Dar es Salaam. Wakati saa chache zimesalia kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, wanahakati wa Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wameendelea kuhamasisha ushiriki wa wanawake kwenye uchaguzi.
Agness Benedicto, mwanaharakati wa Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Mabwepande, ni mfano wa mafanikio ya juhudi hizo ambaye ni miongoni mwa wagombea.
Katika Kata ya Mabwepande pekee, wanawake 45 wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, huku saba kati yao wakiwania nafasi ya uenyekiti.
Asha Daudi, mjumbe wa Kituo cha Taarifa na Maarifa, anasema kuwa licha ya wanawake kujitokeza kugombea wanawake wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na rushwa ya ngono na ukosefu wa fedha za kampeni.
“Rushwa ya ngono na ukata wa fedha ni changamoto kubwa. Wanawake wanashindwa kumudu gharama za kampeni, hali inayopunguza idadi yao katika uchaguzi,” amesema Asha.
Katibu Msaidizi wa Kituo hicho amesema katika mtaa wake, wanawake 10 walijitokeza kugombea nafasi mbalimbali, huku wanaume wakiwa ni 20.
Uchambuzi wa ushiriki wa wanawake
Ripoti ya TGNP inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wanawake wanaotamani kushiriki siasa wanakumbwa na changamoto za kifedha, huku asilimia 40 wakikabiliwa na vikwazo vya kijamii kama vile mila potofu na ukosefu wa elimu.
Pia, utafiti wa Baraza la Wanawake Tanzania (BAWATA) umeonyesha kuwa vyama vya siasa vina nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko kwa kuwajengea uwezo wanawake kupitia mafunzo na ruzuku za moja kwa moja.