Dodoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetahadharisha mambo matatu kwa benki za biashara na Watanzania wakati wa shughuli ya uondoaji wa noti za zamani katika mzunguko wa fedha nchini.
Mambo hayo ni benki za kibiashara kuwa makini katika alama za usalama ili kuepuka noti bandia wakati wa urejeshwaji wa noti hizo na kuhakikisha kigezo cha ubora wa asilimia 75 wa noti hizo kinatimizwa.
Kwa upande wa wananchi, BoT imewataka kuwaepuka matapeli watakaopita kukusanya fedha hizo mitaani kwa kigezo cha kuwatoza gharama za kuwabadilishia.
Meneja Huduma za Kibenki na Sarafu Tawi la BoT la Dodoma, Nolasco Maluli, amesema hayo leo Jumanne, Novemba 26, 2024 wakati akizungumza na wawakilishi wa benki za biashara.
Akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa Benki ya NMB, Amos Mbusi aliyetaka kufahamu BoT, wanazungumziaje baadhi ya watu wanaoweza kutumia shughuli hiyo kupita mitaani na kuwabadilishia watu noti hizo kwa kutaka malipo.
Akijibu swali hilo, Maluli amewataka wananchi kuachana na njia za mkato katika shughuli hiyo ya kuondosha noti hizo na badala yake kufika kwenye taasisi za fedha zilizodhibitishwa na BoT.
Amewataka kwenda benki ambapo watabadilishiwa fedha zao kwa thamani ile ile ya fedha walioiwasilisha na wasikimbilie kwa vishoka wanaoweza kuwatoza gharama.
“Benki haziko mbali sasa hivi, karibu wananchi wote wanafikia huduma za kibenki, labda tuwaongezee kwa sababu mabenki mpo hapa muwape elimu mawakala wenu wawasaidie wananchi kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeshuka sana kwa wananchi,” amesema.
Aidha, Maluli amewatadharisha benki za kibiashara kuzingatia alama za usalama ambazo ziko katika fedha hizo kuepukana na noti bandia kwenye shughuli hiyo.
Amesema kwa wale watakaopata changamoto kwenye alama za usalama katika noti hizo kuwasiliana na BoT kwa msaada.
Amesema mwaka 2023, kuna mtu kutoka Mkoa wa Morogoro ambaye alikuwa akitaka kubadilisha noti za Sh500 ambazo zilikuwa bandia.
Meneja Msaidizi wa Sarafu tawi la BoT, Dodoma, Matilda Luvinga amezitaka benki hizo mbali na kuwa makini na noti bandia, waangalie ubora wa noti zinazopokewa ambao unatakiwa kuwa ni asilimia 75.
“Kama atatokea mtu ambaye ana fedha ambazo zina upungufu kwa madai ya kuuungua na moto basi aje na barua kutoka Serikali ya mtaa iliyogongeshwa muhuri kuwa alipata changamoto hiyo. Utatoa photocopy (nakala) na kisha kuambatanisha na fedha hizo utakavyozirejesha,”amesema.
Oktoba 24, 2024, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba alitoa taarifa kuhusu zoezi la ubadilishaji wa noti hizo linalotarajiwa kuanza Januari 6, 2025 hadi Aprili 5,2025 katika ofisi zote za Benki Kuu na benki za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawa sawa na kiasi kitakachowasilishwa.
Noti hizo zinazoondolewa ni za Sh20, Sh200, Sh500, Sh1,000, Sh2,000, Sh5,000 na Sh10,000 zilizotolewa kuanzia mwaka 1985 hadi 2003 pamoja na noti za Sh500 iliyotolewa mwaka 2010.