Tumekwisha kuifikia siku tuliyoisubiri kwa hamu toka siku nyingi zilizopita. Siku ya kuwachagua viongozi wetu wa mtaani watakaoiwakilisha Serikali kuu milangoni mwetu. Siku tuliyokuwa tukimwomba Mungu usiku na mchana ipite kwa amani, na matokeo yake yakabaki kuwa neema kwetu sote. Ingawa baadhi yetu wanaichukulia siku hii kama vita, lakini ni vita vilivyo vyema kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mimi naiona siku hii kuwa na unyeti unaofanana na imani. Kama jinsi tunavyofunga kiimani kwa kuombea jambo muhimu, inabidi kufunga kwa ajili ya kuombea uchaguzi. Au kama vile tunavyonuiza kabla ya mfungo, inatupasa kunuiza mema kabla ya siku ya uchaguzi. Ieleweke kuwa mtu anayekwenda kuchaguliwa anatarajiwa kuwa mtiifu, mnyenyekevu na mwenye hofu ya Mungu. Kama sivyo basi tumeramba garasa.
Pale mwanzo hakukuwa na kiongozi aliyechaguliwa au kuteuliwa bila ridhaa ya Mwenyezi Mungu. Ni kwa sababu mtu huyo alikwenda kuhusika moja kwa moja na viumbe wa Mungu. Alikwenda kusimamia na kutenda haki mbele za waja wake Mungu, hivyo tunasema alikwenda kufanya kazi ya Mungu. Ndiyo maana uongozi si ujanja, bali ni karama. Ni wito.
Pamoja na kwamba hivi leo viongozi wa mitaa wanapitishwa kwa ridhaa ya vyama vya siasa, lakini mara wanapochaguliwa huapishwa mbele za Mungu huyohuyo kwa kupitia Katiba ya Jamhuri na misahafu mitakatifu. Ingelikuwa tofauti basi wangeapishwa kwa nembo za vyama vyao. Hii inaakisi ni namna gani viongozi wetu wanapewa dhamana ya kumwakilisha Mungu hapa duniani, na si kujali maslahi yao na vyama vyao.
Katika zama zilizopita, viongozi walipatikana kwa mbinde kwelikweli. Hakukuwa na figisu za rushwa wala kampeni chafu. Nakumbuka usemi wa zamani usemao “Mke wa Kaizari hatakiwi kuwa na waa”. Usemi huu ulimuasa kiongozi wa Taifa kubwa la Rumi kwa wakati ule, kuwa makini na watu wanaomzunguka. Kwa vile uongozi ni taasisi huria, ovu lolole likitendwa na yeyote anayemhusu kwa namna yoyote humuathiri.
Kwa tahadhari kuu, kiongozi alitahiniwa vikubwa kabla ya kupewa hatamu za nchi. Kule Misri, uchaguzi wa Farao ulifanyika baada ya mafarao watarajiwa kufanyishwa mitihani migumu ya muda mrefu. Mmoja wa mitihani hiyo ulikuwa ni wa kupasua makasiki saba kwa macho. Wakati mtahiniwa akikaza macho juu ya kasiki kwa lengo la kulipasua, wapinzani wake walilikazia kwa lengo la kuliimarisha lisipasuke.
Hivi sasa uchaguzi umekuwa ni manufaa ya vyama kuliko wapigakura. Watu wamekosa hofu ya Mungu na kutukuza kaulimbiu ya Julius Caesar “Veni, Vidi, Vici” (Nimekuja, Nikaona, Nikachukua). Watu huutamani uongozi na kutoka huko watokako, wakaja kuona maendeleo yaliyopiganiwa na waasisi bega kwa bega na wananchi, kisha huchukua kwa mtindo wa ufisadi na kuondoka zao.
Binadamu hatuishiwi na kefule. Kule bondeni Rais alimteua jambazi mstaafu kuwa Waziri wa Michezo. Pamoja na wananchi kulalamika kuwa hasidi hawezi kuacha hila, lakini Rais akawaambia “shetani akizeeka hugeuka malaika”! Ni wazi alimtaka kiongozi huyo kwa maana yake akiwaacha wananchi wahanga wa bwana huyo wakirudi nyuma ya jitihada za maendeleo kwa hatua kadhaa. Walijisemea “samaki mmoja akioza…”
Hapa nyumbani pamoja na tume ya uchaguzi kuongezewa jina la “huru na haki”, lakini bado tulikosa kuandaa uchaguzi huu kuwa huru na wa haki. Wafuasi wa chama tawala walianza mapema kuwagomea wateule wao walioidhinishwa na tume. Wapinzani wao wakagomea utaratibu wa kuchukua na kurudisha fomu uliowekwa na tume. Kiujumla wapigakura wote walishangazwa na mchakato mzima wa kujiandikisha.
Dalili ya mvua ni mawingu, na penye moshi hapakosi moto. Tunatarajia malalamiko mengi mara baada ya uchaguzi huu, lakini kama kawaida tutakumbushwa kuachana na yanayopita na kuganga yatakayokuja mbele. Lakini hii itakuwa ishara ya makovu kurudia kuwa vidonda katika chaguzi zijazo. Hali ikiendelea hivi kila Mtanzania atachoka. Na hakuna anayeweza kumzuia kila Mtanzania.
Tusijizime data kuwa uchaguzi huu ni utangulizi wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Wapo watakaojifunza makosa ya wenzao na kuingia na mbadala wake kwenye uchaguzi mkuu, lakini pia wapo watakaoona zilipo nyufa zilizotumika na wadudu na kuziziba wakati huo. Mambo hayatakuwa rahisi kama inavyodhaniwa, na pengine hakutakuwa na utulivu.
Wakati mwingine kambi ya upinzani inafanya makosa ambayo ingeweza kuyaepuka. Ukitazama kwa makini utagundua kuwa ni rahisi sana kwa mdogo kukosea anapomwona mkubwa wake nyumbani akifanya makosa. Lakini panapokuwa na wakubwa wenye tahadhari mbele ya watoto au wadogo zao, ni aghalabu kwa wadogo kufanya makosa ya kizembe.
Hivyo tunategemea na tunaiomba Serikali isirudie makosa ya mwanzo wala kuongeza makosa mapya. Yeyote atakayebainika kwenda tofauti na kanuni achukuliwe hatua za kinidhamu. Tukioneana aibu ndio tutakuwa tukimtengenezea shetani njia ya kuongoza uchaguzi, na Taifa letu litakosa kibali mbele za Mwenyezi Mungu. Mungu Ibariki Tanzania.
Nawatakia nyote uchaguzi mwema ulio huru na wa haki.