KONA YA MALOTO: Tuingie ndani ya kongamano la miezi sita ya Makonda Arusha

Jumapili, Novemba 17, 2024, ukumbi wa Simba, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alikusanya wanahabari kwa mazungumzo marefu. Agenda ilikuwa kutoa ripoti ya ufanisi wake ndani ya miezi sita tangu alipoteuliwa na kuapishwa kuongoza mkoa huo.

Arusha ina wanahabari wa kutosha wenye kuwakilisha vyombo vya Arusha na vile vya kitaifa. Makonda alikusanya wanahabari kutoka Dar es Salaam, tena wale maarufu. Bila shaka, alikusudia kulifanya tukio lake liwe kubwa, kwa maana lingepata matokeo chanya kwenye vyombo.

Je, nani alilipa gharama zote hizo? Vyombo vya habari vinavyolia hali ngumu ya kiuchumi, ndivyo vilisafirisha wafanyakazi wao kwa sababu ya Makonda kutimiza miezi sita Arusha ni jambo kubwa? Vipi, ni Makonda mwenyewe ndiye alibeba gharama zote ili kuhakikisha jambo lake linachukua nafasi pana na anakuwa gumzo la siku au wiki?

Kama Makonda ndiye aliyebeba gharama, pesa alitoa wapi? Mkoa wa Arusha una bajeti kubwa kuliko mikoa mingine? Mbona wakuu wa mikoa mingine hawafanyi tafrija za maadhimisho ya uongozi wao? Kuna wakuu wa mikoa wana miaka katika maeneo yao, kwa nini wao hawaiti wanahabari kutoka Dar es Salaam kwa bajeti ya mkoa ili wapambe vyombo vya habari?

Makonda alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alikuwa akimwaga fedha kuliko wakuu wa mikoa wengine. Alikwenda Klabu ya Simba na kutoa Sh20 milioni. Sh10 milioni kwa golikipa Aishi Manula na Sh10 milioni kwa wachezaji wengine. Alikwenda Yanga na kutoa eneo kubwa Kigamboni kwa ajili ya timu hiyo kujenga uwanja wa mpira.

Aliahidi Sh10 milioni kwa kila mchezaji wa Taifa Stars kwa kufanikiwa kufuzu Afcon 2019. Halafu alisafiri kwa ndege daraja la biashara (business class) kwenda Misri kuwahamasisha wachezaji wa Stars kwenye Afcon 2019. Ikaelezwa kuwa akiwa Misri, aliwafanyia ‘shopping’ ya viatu vipya, kila mchezaji na jozi yake.

Aliwajibu polisi Dar es Salaam kuwa asingewapa magari ya thamani ndogo ya Toyota IST kwa sababu hayana hadhi. Alisema, IST ni magari ambayo watu huhongwa. Aliwaahidi polisi kuwanunulia magari yenye hadhi. Alifafanua kwamba ni lazima awape polisi magari ya bei kubwa.

Makonda aliahidi kuanzia Julai mpaka Desemba 2019, angetoa Sh120 milioni kuwawezesha watoto wa kimaskini waliokuwa na matatizo ya moyo, ili wafanyiwe upasuaji kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kwa wastani, kila mwezi ni Sh20 milioni.

Mwezi wa Ramadhani mwaka 2019, Makonda alifuturisha walemavu kwa namna ya kifahari kabisa. Aligawa bidhaa za kutengenezea futari kwa maelfu ya watu. Na hayo ndiyo yamekuwa maisha ya Makonda, kunyoosha mkono na kusaidia watu mbalimbali, wagonjwa, walemavu, maskini na makundi mengine.

Chukua mfano; kwenye hafla ya kuichangia Yanga, Waziri Mkuu alitoa mchango wa Sh10 milioni. Makonda alitoa uwanja Kigamboni. Yapo mengi Makonda ameyafanya kuthibitisha utoaji wake. Swali ni hili; fedha na rasilimali ambazo Makonda hutoa, kama ni za Serikali, mbona wakuu wa mikoa wengine hawatoi kama atoavyo yeye? Tuseme Makonda ni mkarimu kuliko wakuu wengine wa mikoa?

Je, Makonda ni mjanja sana, kwa hiyo hutumia vizuri bajeti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufanya anayoyafanya? Au kuna tofauti kubwa ya bajeti kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa chini ya Makonda na wakuu wengine? Alipokuwa Dar es Salaam alifanya mengi, sasa Arusha ameanza kutikisa.

Dar es Salaam hadi Arusha, mbona wakuu wa mikoa waliomtangulia hawakuwahi kuwa na kasi ya utoaji kama aliyonayo Makonda? Vipi Makonda ni tajiri mwenye pesa nyingi, kwa hiyo anatumia rasilimali zake binafsi?

Je, Makonda ana marafiki wema wenye fedha ambao humchangia kufanikisha agenda zake? Kufanikisha kongamano la miezi sita kama la Makonda AICC, inahitaji fedha nyingi. Kulipia wanahabari usafiri, malazi hoteni, chakula na posho. Jumlisha chakula na vinywaji kwa mamia waliohudhuria. Hii ni bajeti ya mkuu wa mkoa?

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akizungumza alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), jijini Arusha leo Novemba 17, 2024 wakati akiwasilisha ripoti ya miezi sita ya utendaji kazi wake katika nafasi hiyo mkoani humo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Wakati tunajiuliza maswali hayo, tusisahau sakata la “fenicha za walimu”, zilizoibua mzozo Bandari ya Dar es Salaam kati ya Makonda na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, wakati huo akiwa Waziri wa Fedha. Makonda alitaka zitoke kwa sababu ni za msaada kwa ajili ya walimu. Mpango alisisitiza lazima zilipiwe kodi.

Sehemu kubwa ya kongamano lake la miezi sita, aliitumia kujisafisha kwa kashfa mbalimbali zinazomkabili. Tukio lake la kuvamia ofisi za Clouds Media Group (CMG) na mitutu ya bunduki mwaka 2017, tuhuma za kuhusika na shambulio la risasi dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, vilevile kupigwa marufuku kukanyaga Marekani.

Makonda alisema, CMG ilikuwa familia yake na alikwenda kusimamia uhariri wa kazi zake. Swali, mkuu wa mkoa ana ofisi na wasaidizi wake. Makonda alitamka wazi kwamba ndani ya CMG alikuwa na kompyuta zake na wasaidizi wake.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Utafiti CMG, Ruge Mutahaba, alisema Makonda aliwavamia ili kushinikiza maudhui yaliyokataliwa na uongozi, yarushwe kwenye kipindi cha Shilawadu, Clouds TV. Hii dhahiri, kongamano la miezi sita lilibeba agenda ya kujitakasa kijamii na kisiasa. Suala uhusika wa Makonda na shambulio la Lissu Septemba 7, 2017, kinahitaji vyombo kufanya uchunguzi, si Makonda kujisafisha wala Lissu kutoa tuhuma bila ushahidi. Ni kama ambavyo Makonda alisema kupigwa kwake marufuku kwenda Marekani sababu ni vita aliyoianzisha dhidi ya ushoga.

Inafahamika, Makonda alipewa adhabu hiyo kipindi ambacho Marekani ilikuwa ikiongozwa na Rais Donald Trump. Isingekuwa sahihi kumwadhibu mtu anayefanya jambo analopenda.

Related Posts