Shinyanga. Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Alexius Kagunze, amesema baadhi ya vituo vya wazi ambavyo haviko kwenye majengo ya umma, havijabandika majina isipokuwa wapiga kura wanaangalia kwenye orodha iliyopo kwa wasimamizi kisha wanapiga kura.
Hii ni tofauti na hali ilivyo kwenye vituo vilivyopo kwenye majengo ya umma ambapo majina yamebandikwa na mpiga kura anahakikisha kisha kupiga kura.
“Hali hiyo haijaathiri, ndiyo maana watu wanaendelea kupiga kura, ila sikatai changamoto ndogondogo zipo na tunaendelea kuzitatua kwa haraka,” amesema Kagunze leo Novemba 27,2024.
Awali Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami akiwa kituo cha wazi Ikulu Kata ya Lubaga alilalamikia kutobandikwa majina katika baadhi ya vituo akidai kuwa ni kutowatendea haki wananchi.
Hata hivyo, wakati Mnyawami alalamikia majina kutobandikwa, mpaka Saa 5 asubuhi, Mwananchi ilikuwa imepita kwenye baadhi ya vituo na kushuhudia wapiga kura waliojitokeza ni wachache na vituo vingine vikiwa havina watu.
Jane Peter mkazi wa Masekelo amesema utaratibu wa kupiga kura ni mzuri kutokana na kazi hiyo kuwa rahisi.
Amesema mbali na upungufu huo, maandalizi mengine yameenda vizuri hali iliyosaidia watu kuendelea kupiga kura na kuondoka kwenda kufanya shughuli nyingine.
Akizungumza baada ya kupiga kura, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amewataka wananchi kutumia muda uliobaki kwenda kupiga kura mapema ili wachague viongozi wao.
Amesema vituo vyote vimefunguliwa kwa wakati huku akiwasihi wananchi waendelee kupiga kura kwa utulivu.
“Ukimaliza kupiga kura nenda kaendelee na shughuli nyingine za kulijenga Taifa huku ukisubiri kutangazwa kwa matokeo,” amesema Anamringi.