Viongozi wapongeza makubaliano ya usitishwaji vita Lebanon – DW – 27.11.2024

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron wamesema katika taarifa yao ya pamoja kabla ya kuanza kutekelezwa kwa makubaliano hayo ya usitishwaji mapigano kuwa yatawezesha kuilinda Israel dhidi ya tishio la kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah na makundi mengine ya kigaidi yanayofanya kazi nchini Lebanon na pia yataweka mazingira ya “utulivu wa kudumu”.

Viongozi hao wameendelea kusema kuwa Marekani na Ufaransa zitafanya kazi ya kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kikamilifu na kuongoza juhudi za kimataifa za kuimarisha uwezo wa jeshi la Lebanon. Biden alipokea vyema makubaliano hayo aliyoyaita “habari njema” na kusisitiza kuwa Marekani itaongoza pia juhudi mpya za kuwezesha makubaliano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Palestina la Hamas huko Gaza. Macron amesema  usitishaji vita nchini Lebanon  unapaswa “kufungua njia” ya kuvimaliza vita vya Gaza.

Kauli za viongozi wa Israel, Lebanon na Iran

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Uncredited/Israeli Government Press Office/AP/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemshukuru rais wa Marekani kwa ushiriki wake katika kufanikisha makubaliano hayo lakini akasema amefurahishwa zaidi na uelewa wa rais Biden kwamba serikali ya Israel itakuwa na uhuru wa kuchukua hatua muhimu za kuyatekeleza makubaliano hayo. Kabla ya Israel kuidhinisha mpango huo, Netanyahu alisema kuwa kudumu kwa mpango huo wa usitishaji vita kutategemea na kile kitakachotokea nchini Lebanon, na kwamba mpango huo utaiwezesha Israel “kuzidisha” shinikizo kwa Hamas na kushughulikia vyema “kitisho cha Iran”.

Soma pia: Israel yaishambulia Beirut kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano

Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon Najib Mikati amesema mpango huo ni hatua muhimu ya kuelekea kurejesha utulivu katika eneo hilo, huku akiyashukuru mataifa ya Ufaransa na Marekani kwa kusimamia mchakato huo. Mikati hata hivyo amesisitiza dhamira ya serikali yake ya “kuimarisha uwepo wa jeshi lake katika maeneo ya kusini mwa Lebanon”.

Iran ambayo inayaunga mkono makundi ya Hezbollah na Hamas, ilipongeza pia mpango huo ilioutaja kuwa “mwisho wa uchokozi” wa Israel nchini Lebanon. Msemaji wa waziri wa mambo ya nje Esmaeil Baghaei amesema Tehran inathibitisha uungaji mkono thabiti kwa taifa la Lebanon, serikali yake pamoja na kundi la Hezbollah.

Miito yatolewa kuhusu kuvimaliza vita vya Gaza

 Jabalia I Raia wa Gaza wakishuhudia uharibifu utokanao na vita kati ya Israel na Hamas
Raia wa Gaza wakishuhudia uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Israel huko JabaliaPicha: Omar AL-QATTAA/AFP

Afisa wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema hivi leo kuwa kundi hilo limeridhia haki ya Lebanon kufikia makubaliano ambayo yanalinda watu wake, na kusema kuwa wako tayari pia kwa mpango kama huo huko Gaza. Afisa mwengine wa Hamas amesema wako tayari kwa makubaliano ya  usitishwaji vita Gaza  lakini akasema kuwa bado Israel ndio haijaafiki.

Waziri wa Mambo ya nje wa Australia Penny Wong ametaka kusitishwa vita katika eneo hilo.  

“Tunapongeza usitishaji vita kati ya Israel na Hezbollah. Watu wa Lebanon na wale wa Israel watapokea vyema usitishaji huu wa vita. Ninachoweza kusema ni kwamba tunatumai kuwa hii itakuwa kichocheo cha kuwezesha usitishaji vita mpana zaidi katika eneo hilo. Na tunasubiria siku ambayo kutakuwa pia na usitishaji vita huko Gaza,” alisema Wong.

China na Iraq zimepongeza pia hatua hiyo na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kumaliza pia vita vya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Vyanzo: (AP, AFP, DPAE)

 

Related Posts