Rais Samia: Masanduku yatakavyosema ndivyo matokeo yatakavyokuwa

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amepiga kura kuwachagua viongozi wa serikali ya Kijiji cha Chamwino kilichopo Wilaya ya Chamwino jijini hapa, huku akisisitiza wananchi kupiga kura kwa maelewano na kuwa masanduku yatakavyosema ndiyo matokeo yatakavyokuwa.

Rais Samia amebainisha hayo wakati akipiga kura leo Jumatano Novemba 27, 2024 katika kituo cha Sokoine kilichopo katika kijiji hicho. Amewataka watu wote wenye sifa wajitokeze kwenda kupiga kura.

Amesema anadhani Watanzania wataitikia wito wake na kwamba leo ameona watu ni wengi kidogo (katika kituo cha Sokoine).

“Wito wangu wa pili ni kwamba kura hizi ni mtindo wetu wa kidemokrasia na utamaduni wetu wa kisiasa, waende (Watanzania) wakaufanye (uchaguzi) kwa usalama na amani,  wasivunje amani yetu. Wakapige kura kwa maelewano na masanduku yanavyosema ndio hivyo matokeo,” amesema.

Amesema matumaini yake ni kuwa Watanzania watachagua uongozi wao katika ngazi za maeneo yao kwa salama na vizuri na watawachagua watu wenye uwezo wa kufanya kazi zao.

Rais Samia alifika katika kituo hicho saa 5:15 asubuhi na kupiga kura saa 5.19 baada ya kusubiri watu kadhaa waliomtangulia kupiga kura.

Related Posts