Dar es Salaam. Dk Faustine Ndugulile alikuwa daktari wa tiba aliyehitimu katika afya ya umma na taaluma ya mikrobiolojia ya tiba.
Pia Dk Ndugulile alikuwa mwanasiasa aliyehudumu kama mbunge na amekuwa waziri kwa nyakati tofauti.
Dk Ndungulile alizaliwa wilayani Mbulu mkoani Manyara Machi 31, 1969. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule Groombridge iliyopo Harare nchini Zimbabwe mwaka 1976 na kuhitimu 1982.
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi aliendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Prince Edward, Harare nchini humo kuanzia mwaka 1982 mpaka 1986.
Baada ya kufaulu kidato cha nne, Ndungulile aliendelea na elimu ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Tambaza iliyopo jijini Dar es Salaam, Tanzania mwaka 1987 mpaka 1989.
Mwaka 1990 mpaka 1997 Ndungulile alifanya shahada yake ya kwanza ya udaktari (MD) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Aliendelea na masomo akichukua shahada ya uzamili (MMED) katika chuo hicho aliyohitimu mwaka 2001.
Kati yam waka 1997 na 1998, Ndugulile alikuwa daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na pia alikuwa mtaalamu wa mikrobaiolojia hadi mwaka 2004 alipoteuliwa kuwa meneja wa programu katika Wizara ya Afya.
Mwaka 2004 hadi 2006 alihudumu kama mkuu wa kitengo cha uchunguzi katika Wizara ya Afya na mwaka 2007 hadi 2010 alikuwa mshauri wa afya katika taasisi ya Udhibiti wa Magonjwa (CDC) nchini Afrika Kusini.
Kati ya mwaka 2006 hadi 2007 pia alihudumu kama Meneja wa programu katika Mpango wa damu salama.
Dk Ndugulile alijiunga na siasa mwaka 2010 na amekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, Tanzania hadi mauti yake.
Alihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii, na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ukimwi na Matumizi ya Dawa za Kulevya.
Aliongoza Kamati ya Ushauri ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuhusu Ukimwi, Afya ya Mama na Mtoto yenye makao yake Geneva kati ya mwaka 2015 na 2017. Kati ya mwaka 2008 na 2016, Dk Ndugulile alikuwa mwanachama wa Baraza la Utawala la Jumuiya ya Kimataifa ya Ukimwi (International AIDS Society) yenye makao yake Geneva.
Aidha, Dk Ndugulile alikuwa mwanachama wa Bunge la Afrika (2015-2017), mwanachama wa Jumuiya ya Wataalamu wa Microbiolojia ya Marekani (ASM), Chama cha Afya ya Umma Tanzania (TPHA) kama Katibu Mkuu na baadaye Mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge wa Tanzania wa Kupambana na Ukimwi (TAPAC).
Dk Ndugulile aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee kati ya mwaka 2017 na 2020.
Baada ya kuanzishwa kwa Wizara mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Desemba 2020, Dk Ndugulile aliteuliwa kuwa Waziri wake wa kwanza.
Alichaguliwa kuwa Mkurugenzi kikanda wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO), katika kikao cha 74 cha Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO kilichofanyika nchini Congo Brazzaville Agosti 26 hadi Agosti 30, 2024 na alitarajiwa kumrithi Dk Matshidiso Moeti wa Botswana aliyemaliza muda wake.