Wasota kwa saa nne kusubiri karatasi za kupigia kura

Malinyi. Baadhi ya wananchi walijitokeza kupiga kura katika kituo cha Makerere, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, mkoani Morogoro, wamelazimika kusubiri hadi saa nne asubuhi bila kupiga kura, kutokana na ukosefu wa karatasi za kupigia kura.

Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Malinyi, Khamis Katimba amesema changamoto hiyo ilitokea mapema leo asubuhi baada ya wananchi kufika kituoni hapo.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatano Novemba 27, 2024, Katimba amesema karatasi zilizopelekwa zilikuwa chache ikilinganishwa na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha.

“Kituo kilikuwa na zaidi ya wapiga kura 300, lakini karatasi zilizoletwa zilikuwa takriban 200. Tumelazimika kuongeza zaidi ya karatasi 100,” amesema Katimba.

Hata hivyo amesema baada ya changamoto hiyo kutatuliwa upigaji kura katika kituo hicho unaendelea.

“Ila watu ni wengi na foleni bado ndefu, lakini hata uhakiki wa majina nao kidogo una changamoto inayochangiwa  na baadhi ya wapigakura kutojua kusoma, inabidi wawaombe ndugu zao ambao nao ni wapiga kura wawatafutie majina yao,” amefafanua Katimba.

Katika maeneo mengine ikiwamo Manispaa ya Morogoro, changamoto za orodha za wapiga kura kutosomeka vizuri zimeripotiwa.

Akizungumza na Mwananchi, Mwajuma Said, mmoja wa wananchi waliofika kituo cha kupigia kura  Tushikamane, amesema majina yanasomeka kwa shida akidai maandishi ni madogo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Uchaguzi wa Mkoa wa Morogoro, Jacob Kayenge amesema changamoto hiyo imetafutiwa ufumbuzi kwa lengo la kuhakikisha kila aliyejitokeza anapata haki yake.

Kayenge amesema Mkoa wa Morogoro una jumla ya wapiga kura 1,806,190 waliojiandikisha katika vituo 3,494 vya kupigia kura, huku vyama 17 vya siasa vikiwa na wagombea 19,000.

Related Posts