Kiongozi Chadema alalama wapigakura wasio sahihi kupiga kura

Dodoma. Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dodoma, Aisha Madoga amesimamisha kwa muda shughuli za uchaguzi wa serikali za mitaa kwenye kituo cha Site One kilichopo Mlimwa jijini Dodoma, kwa madai kuwa kuna watu siyo wakazi wa mtaa huo, wameruhusiwa kupiga kura wakati majina yao hayapo kwenye orodha ya wapigakura.

Akizungumza kwa njia ya simu leo Jumatano Novemba 27, 2024, Aisha amesema licha ya yeye kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma, pia ni wakala wa ziada, hivyo alipopata taarifa kuwa kuna watu wanapiga kura bila kuwa kwenye daftari la wapigakura, aliamua kufuatilia taarifa hizo ili kuujua ukweli wake.

Awali, kuna video iliyokuwa inamwonyesha mwenyekiti huyo na baadhi ya wanawake wakifanya fujo kwenye kituo cha kupigia kura na kutaka kulichana daftari la wapigakura, huku wakitukana matusi kwa madai kuwa kuna watu wanaopiga kura na wakati siyo wakazi wa mtaa huo.

Kutokana na hali hiyo askari Polisi aliyekuwepo eneo la tukio alimwondoa mwenyekiti huyo ili kupisha wananchi wengine kuendelea kupiga kura.

Aisha amesema aliamua kwenda kwenye kituo hicho na alipofika alimwambia dereva wake, msaidizi wake na rafiki yake mmoja ambao siyo wakazi wa mtaa huo waende wakapige kura kuona kama wataruhusiwa, walipopanga foleni walipewa karatasi za kupigia kura na walipiga kura bila kukaguliwa majina yao kama kweli yapo kwenye daftari la wapiga kura.

“Wakala alimwambia msimamizi msaidizi wa uchaguzi kuwa hawawafahamu hao watu lakini yeye aliwaruhusu kupiga kura na kuweka tiki kwenye jina ambalo siyo la mpiga kura….kwa kweli hali ile ilinifanya nimtake msimamizi huyo wa kituo kunionyesha jina la aliyepiga kura lakini alishindwa na alitaka kulificha daftari aliloweka tiki,” amesema Aisha.

Amesema kutokana na tukio hilo alilazimika kuzuia watu wasiendelee kupiga kura mpaka pale watakapojiridhisha kuwa ni wakazi wa eneo hilo, lakini hata hivyo aliondolewa na askari aliyekuwa kwenye kituo hicho ili kupisha upigaji kura uendelee.

Mbali na hilo Aisha amesema kuwa wamekamata kura feki kwenye kata za Iyumbu na Mbabala ambapo walikuta masanduku ya kupigia kura tayari yana kura, wakati watu walikuwa bado hawajaanza kupiga kura.

Amesema taarifa za kukamatwa kwa masanduku hayo zipo Polisi kwani wahusika walikamatwa na kupelekwa kituoni.

Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Dodoma Mjini, Dk Frederick Sagamiko amesema hajapata malalamiko yoyote kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika leo nchini.

Amesema kama kuna mtu yeyote ambaye ana malalamiko ayafikishe ofisini kwake ,kwani mpaka sasa hajapata taarifa zozote za watu kushindwa kupiga kura, kukosa karatasi za kupigia kura au kituo kutofunguliwa kwa wakati.

“Hali ni shwari mpaka sasa hakuna changamoto yoyote iliyozuia watu kupiga kura kila mahali hali ni shwari na watu wamejitokeza kwa wingi…..hao ambao wana malalamiko waambie waje ofisini kuleta malalamiko yao leo tupo wazi na mimi nipo hapa kupokea malalamiko yoyote kuhusiana na uchaguzi huo,” amesema Dk Sagamiko.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Geoge katabazi kuzungumzia kukamatwa kwa watu waliokuwa na kura feki hazikuzaa matunda, baada ya simu yake kupokelewa na msaidizi wake aliyesema kuwa yuko kwenye kikao cha dharura.

Related Posts