Akihutubia maelfu ya watu waliokuja kumlaki jimboni Tanganyika Rais Felix Tshisekedi alizungumzia ajenda 6 za ajira, usalama, ustawi wa jamii, uchumi, Kilimo pamoja na Utawala bora, ahadi alizotoa wakati wa kampeni ya uchaguzi uliopita. Ameeleza kuwa serikali inajitahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.
Kiongozi huyo pia amezishtumu baadhi ya nchi bila ya kuzitaja majina kwa kuingilia kati masuala ya ndani ya taifa hilo, na kuwatahadharisha vijana juu ya kushawishiwa.
“Tuna maadui wengi waliopo katika nchi jirani na ambao waliweza kupata ushirikiano ndani ya nchi yetu. Tuna baadhi ya wananchi ambao wamejitolea kuivuruga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.”
Tshisekedi abainisha mpango wa kuimarisha ulinzi jimboni Tanganyika
Amesema wameamua kuimarisha ulinzi hivi na kwamba hivi karibuni wataweza kushuhudia brigedi nzima au brigedi mbili za jeshi la jamhuri zinashuka, wanahitaji amani, na ni kwa amani watafanikiwa kuiendeleza nchi yeo. Tayari wamechukua hatua ya kupunguza bei ya vyakula vya msingi, kiwango cha Faranga ya Kongo ikilinganishwa na dola.
Aidha rais amewatolea mwito vijana kutafuta fursa za kujiajiri kwani serikali haiwezi kuajiri watu wote. Mmoja kati ya raia wa Kongo anasema “Kizuri kwangu ni tujitegemee, tulime, Ile imenifurahisha sana” mwengine Omari Athumani anasema “Alichosema cha maana ni kwamba atajitajidi kwaajili ya matatizo ya wanafunzi wa sekondari kuhusu malipo Yao.”
Raia wamtaka rais atimize wajibu wake
Lakini baadhi ya wengine katika jimbo hilo la Tanganyika wameonesha masikitiko yao kwa rais kuwasahahu katika eneo hilo ambalo lina shida kubwa ya kiusalama. Licha ya baadhi ya raia kuchoshwa na ahadi za miaka mingi ambazo hutolewa na viongozi pasina kutimizwa Tshisekedi amesema bado dhamira ya kubadili katiba ipo palepale na kwamba wenye maamuzi ya mwisho ni raia.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Yango Marcelin amesema “Tulikuwa tunafikiria kwamba ni muda kwake kuweza kutekeleza kile ambacho alikizungumzia wakati wa kampeni, jambo moja tu ambalo hakuzungumzia wakati wa kampeni ni kuibadilisha katiba.”
Soma zaidi:Malalamiko ya chama cha majaji DRC
Aliongeza kwa kusema “Isingekuwa na tija kutuzungumzia sisi bali yeye angejikita kututengenezea kile ambacho aliweza kutuahidia. Ukiangalia watu wote wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katiba hawaipatii nafasi kubwa sababu hakuna chakula, Miundombinu Bado hafifu, ajira hakuna, usalama ndo tusizungumze hakuna kabisa. Leo watu wanaozungumzia katiba ni wale wafanya siasa ambao wanajipanga kuweza kuchukuwa madaraka kesho.” Alisema Marcelin.
DW Kalemie