Mvua yatajwa kuharibu orodha ya wapigakura Mwanza, wahaha kupiga kura

Mwanza. Mvua imetajwa kuwa kikwazo kwa baadhi ya wananchi kufika kwenye vituo kwa wakati huku wengine wakidai majina yao kutoonekana vyema kutokana na karatasi zenye orodha yao kulowa.

Mvua hiyo ambayo imeanza kunyesha tangu saa 1:30 muda mfupi kabla ya vituo vya uchaguzi kufunguliwa hadi saa 5:30 asubuhi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza imetajwa kuathiri hiyo.

Mwananchi imezunguka katika vituo mbalimbali mkoani Mwanza, ikiwemo Kituo cha Nyanza Kata ya Mkolani, Bohari Kata ya Butimba, Igombe Kata ya Pamba, Nyamarango Kata ya Luchelele na Kituo cha Uwanja wa Nyamagana wilayani humo na kushuhudia idadi ndogo ya watu huku vingine vikiwa havina watu kabisa.

Vituo vingine ambavyo Mwananchi imefika na kubaini uwepo wa malalamiko ya majina kutoonekana huku wengine wakisema karatasi zimechanwa na mvua, ni Kabambo Kata ya Kiseke na Kitangiri wilayani Ilemela mkoani hapa.

Mkazi wa Kabambo, Levin Alfred amesema kutokana na karatasi zenye majina kulowana amekwama kutambua jina lake, jambo lililomlazimu kupanga foleni kuhakiki jina lake kwenye kitabu maalumu kilichopo kwenye dawati la mawakala.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Zaitun Ally amesema hadi kufikia Saa 9:00 alasiri alikuwa hajaona jina lake, jambo ambalo limefanya aanze kukosa matumaini ya kupiga kura na kumchagua mwenyekiti wa mtaa huo.

“Hadi muda huu nimeangalia jina langu kwenye karatasi sijaliona, karatasi zenye majina zimenyeshewa mvua,” amesema Zaitun.

Katika hatua nyingine, Mkazi wa Nyamalango jijini Mwanza, Amina Issa amesema; “watu ni wachache sana lakini ni haki yangu kupiga kura ndio, maana nimesitisha kufanya kazi zangu ili nitimize wajibu wangu, hivyo hali ya mvua isiwakwamishe wananchi kupiga kura,” amesema.

Kutokana na changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Shaban Itutu ameishauri Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuandaa miundombinu rafiki isiyoathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa ili kutoathiri upigaji wa kura.

Itutu amesema katika kituo alipochipia kura pia kuna malalamiko ya wananchi kukosa majina yao, jambo ambalo huenda likawanyima haki wananchi kuchagua viongozi wao.

Kilio cha mvua hiyo, kimemlazimu, Sijaona Karoli kuiomba Serikali kuongeza muda wa upigaji kura katika uchaguzi huo ili kuruhusu wananchi kutimiza adhma yao ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi katika Halmshauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema pamoja na mvua kunyesha mwitikio wa watu kupiga kura unaridhisha.

Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani humo, Ummy Wayayu amekiri kupokea malalamiko ya baadhi ya wananchi kudai majina yao hayaonekani, na kuwa ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa vituo wachape majina ya kuyabandika kabla muda kumalizika.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira, Anania Kajuni na Timothy Lugoye

Related Posts