Unguja. Katika kipindi cha miaka miwili 2022/23 na 2023/24 Sh17.985 bilioni zimekusanywa Zanzibar katika kodi ya miamala ya simu.
Kiwango hicho ni sawa na wastani wa Sh8.992 bilioni zilizokusanywa kwa mwaka mmoja.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya leo Novemba 27, 2024 wakati akijibu swali la mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman katika mkutano wa 17 wa Baraza la Wawakilishi.
Katika swali la msingi, Dk Mohammed amesema licha ya taarifa kuonyesha kuwapo ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma za mawasiliano ya data, sauti, ongezeko la miamala ya fedha kwa kutumia simu za mkononi na mtandao wa intaneti, bado mgawanyo wa mapato pande zote mbili za Muungano haujawekwa wazi.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuya amesema huduma za miamala ya simu zinatozwa kodi za aina mbili, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa bidhaa ya miamala hiyo.
Sheria zinazotumika katika miamala ya simu kwa upande wa Zanzibar ni Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) namba nne ya mwaka 1998 na Sheria ya Ushuru wa Bidhaa namba nane ya mwaka 2017.
Amesema kodi hizo si za Muungano kwani kila upande una sheria zake ambazo zinasimamia utozaji kodi katika miamala ya simu.
“Katika kipindi cha miaka miwili ya kukusanywa rasmi kodi hii mwaka 2022/23 na mwaka 2023/24 jumla ya Sh17.9 bilioni zimekusanywa,” amesema.
Waziri amsema mapato yanayokusanywa katika simu yanaingizwa katika akaunti za Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na baadaye katika mfuko wa Hazina kama ilivyo kwa mapato mengine ya Serikali yanayokusanywa Zanzibar.
“Badala ya kuingia katika mfuko mkuu wa Hazina Zanzibar zinapangiwa matumizi kama ambavyo bajeti ilivyopitishwa,” amesema.
Amesema ZRA inakusanya kodi katika vyanzo mbalimbali vya mauzo ya bidhaa na huduma za mawasiliano ya simu.
Ameeleza kodi hizo hukusanywa kupitia mfumo wa kielektroniki kwa lengo la kugawanya kodi baina Zanzibar na Tanzania Bara.
“Kwa maana hiyo, mgawanyo wa mapato ya tozo ya miamala ya simu kwa pande zote mbili inatokana na eneo ambalo muamala huo umefanyika,” amesema.
Hata hivyo, katika kusimamia hilo amesema wameandaa mwongozo unaotumika katika ukusanyaji wa tozo kwenye miamala ya simu na pia timu ya wataalamu kujadiliana na kuzitafutia ufumbuzi changamoto.