Makamishna wapya wa Halmashauri kuu ya Ulaya waidhinishwa – DW – 27.11.2024

Makamishna wapya wa Halmashauri hiyo kuu wameidhinishwa kwa kura za wabunge 370 waliounga mkono, 282 waliopinga na 36 waliojiepusha kushiriki katika zoezi hilo.

Baada ya kura hiyo, von der Leyen aliyekuwa na tabasamu, aliwakumbatia wanachama wa timu yake mpya pamoja na baadhi ya viongozi wa kisiasa waliomuunga mkono.

von der Leyen asema hakuna muda wa kupoteza

Kabla ya kura hiyo ya uidhinishaji, von der Leyen aliwaambia wabunge hao wa Umoja wa Ulaya mjini Strasbourg kwamba hakuna muda wa kupoteza na kwamba lazima wawe wakakamavu kwa sababu vitisho ni vikubwa.

Uhuru wa Umoja wa Ulaya unategemea nguvu za kiuchumi 

Mkuu huyo wa halmashauri hiyo ya Umoja wa Ulaya, ameongeza kuwa uhuru wao unategemea zaidi kuliko wakati mwingine wowote nguvu zao za kiuchumi huku akitangaza shinikizo la ushindani ndani ya siku 100, na kuahidi kuongoza binafsi mazungumzo ya kimkakati juu ya mustakabali wa sekta ya magari inayoyumba barani Ulaya.

Bunge la Ulaya lamthibitisha Ursula von der Leyen katika nafasi ya juu

Majukumu makuu ya halmashauri hiyo mpya ni kuangazia vipaumbele vya miaka mitano ijayo.

Majukumu ya makamishna wa Umoja wa Ulaya

Waziri mkuu wa zamani wa Estonia Kaja Kallas anatarajiwa kuwa mwanadiplomasia mkuu wa Umoja huo, huku Andrius Kubilius wa Lithuania akichukua nafasi mpya ya kusimamia harakati za Umoja huo wa Ulaya za ununuzi wa silaha.

Rais wa halmashuri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiwa ziarani  Montenegro mnamo Oktoba 26,2024
Rais wa halmashuri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Rusmin Radic/Anadolu/picture allianc

Stephane Sejourne wa Ufaransa anatarajiwa kusimamia mkakati wa viwanda katika wakati ambapo viwanda vinakabiliwa na changamoto nyingi pamoja na ushindani kutoka China, gharama kubwa za nishati na uwekezaji hafifu.

Ursula von der Leyen achaguliwa kwa awamu ya pili kuongoza Halmashauri ya Ulaya

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Ufaransa atalazimika kufanya kazi na Teresa Ribera wa Uhispania, ambaye ndiye mkuu mpya wa harakati za kugeukia matumizi ya nishati safi pamoja na ushindani ili kuoanisha ukuaji wa kiuchumi na malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Je, Ursula von der Leyen atapata kura anazohitaji?

Halmashauri hiyo kuu ya Umoja wa Ulaya imekuwa katika maandalizi tangu Umoja huo wa nchi 27 ulipofanya uchaguzi mnamo mwezi Juni.

Halmashauri hiyo kuu, bado inasubiri kuidhinishwa na nchi wanachama lakini hatua hiyo inachukuliwa tu kuwa ya utaratibu rasmi.

Viongozi wa Ulaya wahimiza mageuzi ya kiuchumi ya kanda hiyo

Hata hivyo, makamishna hao wapya wanakabiliwa na uwezekano wa kukumbwa na changamoto kubwa za kiuchumi, kijiografia na kisiasa katika muhula wao wa kuhudumu wa miaka mitano.

Halmashauri hiyo itazingatia masuala ya kiuchumi na usalama huku Umoja huo wa Ulaya ukijitahidi kubaki kwenye ushindani wa kiuchumi na China na Marekani, wakati pia ikijihami kwa silaha dhidi ya kitisho kutoka Urusi.

 

Related Posts