Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata watu wanne wakiwemo mawakala wawili wa Chadema na mgombea uenyekiti wa chama hicho, Atanas Ndaki, kwa madai ya kukimbia na boksi lenye karatasi za kura.
Mwingine aliyekamatwa ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Nyamagana, Amos Ntobi kwa madai ya kufanya fujo kituo cha kupigia kura Kabengwe Mtaa wa Mabatini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 27, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema boksi hilo lilikuwa na kura 181 ambazo hazijapigwa.
“Leo (Novemba 27, 2024), saa 1:30 asubuhi katika Wilaya ya Nyamagana kituo cha kupigia kura cha Lwanhima, kituo B, Mtaa wa Mariza kilichopo Shule ya Sekondari Lwanhima, wakala wa Chadema, Edward Otieno Odingi ambaye alikuwa kwenye kituo hicho wakati huo alianza mawasiliano na mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti, Atanas Ndaki.”
“Alipofika kwenye kile kituo, katika hali ya kushangaza, wakala huyo alichukua boksi ambalo lilikuwa na karatasi za kupigia kura na kuondoka nalo akiongozana na mgombea huyo wa Chadema.”
Mutafungwa ameongeza kuwa baada ya askari wa Jeshi la Akiba aliyekuwa katika kituo hicho kumuona anafanya tukio hilo, alianza kumfukuza na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kupitia askari waliokuwa doria maeneo jirani na kituo hicho.
Amesema askari wa jeshi hilo wakishirikiana na mlinzi wa kituo hicho walifanikiwa kumkamata wakala huyo pamoja na mgombea wa uenyekiti kupitia Chadema.
“Na katika kuwakamata waliwakuta na karatasi za kupigia kura ambazo hazijapigiwa. Jeshi la polisi pia tumemkamata mtu mwingine, Ally Hussein, wakala wa kituo cha Lwanhima A,” amesema Mutafungwa.
Akizungumzia sababu za kumkamata Ntobi, Mutafungwa ameeleza kuwa katibu huyo alikuwa akifanya fujo akidai kuwa kituo cha Kabengwe hakipo kwenye orodha ya vituo vya kupigia kura. Mutafungwa amesema uchunguzi wa matukio hayo unaendelea.
Akizungumza kwa simu kuhusu tukio hilo, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, Zacharia Obad amesema si kweli kuwa mawakala hao wamekamatwa na boksi la kura, bali wamegeuziwa kibao baada ya kukamata boksi hilo na kuanza kupiga kelele za msaada.
“Ni waongo. Mawakala ndio wamekamata boksi likiwa lina kura zilikuwa zimepigwa tayari, walivyoanza kupiga kelele wakageuziwa kibao na kukamatwa,” amesema Obad.