KOCHA wa makipa wa Fountaine Gate, Ally Mustapha ‘Barthez’ na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Abalkassim Suleiman wamekiri kusimamishwa na klabu hiyo kwa sababu mbalimbali huku Desemba 6 mwaka huu uongozi ukitarajia kukaa kikao cha kuwajadili.
Barthez na Abalkassim walisimamishwa siku moja baada ya timu hiyo kufungwa na Pamba Jiji mabao 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Novemba 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.
Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, walisema ni kweli wamesimamishwa huku Abalkassim akibainisha kwamba alipokea barua yenye makosa mawili.
“Ni kweli nipo nje ya timu na nilipokea barua ya kusimamishwa kwa kosa la kuondoka kambini bila ruhusa lakini pia natuhumiwa kuwa nilicheza vibaya kwenye mchezo dhidi ya Pamba ambao nilionyeshwa kadi nyekundu wakidai kuwa nilifanya makusudi,” alisema kiungo huyo na kuongeza.
“Baada ya wiki mbili kupita niliwapigia viongozi juu ya sakata hilo niliomba kuonana nao ili wanipe barua ya kuachana na timu kutokana na hayo madai, sikupewa na zaidi wamenitaka nikutane nao tena Desemba 6 mwaka huu kwaajili ya kikao cha kunijadili.”
Kwa upande wa Bartez alisema hafahamu sababu za kusimamishwa kwake bali anachoweza kusema yupo nje ya timu hiyo kwa muda anaendelea na shughuli nyingine.
“Nafikiri watu sahihi wa kuzungumza nao juu ya sababu za mimi kuondoka ndani ya timu ni viongozi, mimi nipo Dar es Salaam kwa sababu nimeondolewa kwenye majukumu yangu sifahamu sababu ni nini,” alisema Barthez ambaye aliwahi kuwa kipa wa Simba na Yanga kabla ya kugeukia katika ukocha.