Musonda kumpisha Dube Yanga | Mwanaspoti

WAKATI Yanga ikiwa kwenye mchakato wa kusaka mbadala wa Joyce Lomalisa ambaye anatajwa kuachwa mwisho wa msimu huu, imebainika kuwa mshambuliaji Keneddy Musonda pia anampisha mtu.

Musonda anamaliza msimu wake wa pili mwishoni mwa msimu huu na hakuna mazungumzo yoyote baina yake na uongozi kwa ajili ya mkataba mpya na inatajwa kuwa atampisha Prince Dube ambaye anapambana kumaliza utata wake na waajiri wake wa zamani, Azam FC.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa uongozi umefanya uamuzi wa kuachana na Musonda mwisho wa msimu na kuendelea na Joseph Guede ambaye ameanza kuonyesha uwezo huku akikiri kuwa wataongeza mshambuliaji mmoja.

“Mkataba wa Musonda unamalizika mwisho wa msimu ni kweli hakuna mazuingumzo mapya hii ni kutokana na uamuzi uliopitishwa na benchi la ufundi kuwa bora kubaki na Guede na kuongeza mshambuliaji mmoja mwenye jicho la kuona goli,” kimesema chanzo hicho

“Tayari uongozi umeanza kufanyia kazi suala la kuongezwa kwa mchezaji eneo la ushambuliaji nafikili muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi sio wakati sahihi kuzungumza masuala ya usajili wakati bado tuna mechi za ligi ambazo kwetu ni muhimu zaidi ili kutetea taji.” 

Mwanaspoti linafahamu kuwa Yanga wamekuwa wanafukuzia saini ya Dube ili aweze kufanya kazi sambamba na Guede ambaye gari limewaka akitupia mabao kwenye kila mchezo na sasa amefikisha matano akimuacha Musonda mwenye mabao matatu, huku taarifa zingine zikidai tayari nyota huyo Mzibambwe ameshamalizana na Yanga na amekabidhiwa mkataba wa miaka miwili.

Dube amefikisha sakata lake la kutaka kuachana na Azam FC katika Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), akipiga kuwa ana mkataba na timu hiyo wa miaka miwili ambao umebaki, huku akitaka mkataba uliobaki usiofika mwaka uvunjwe.

Wakati huohuo, mchezaji kiraka ndani ya Yanga, Farid Mussa anatajwa pia kuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu ujao baada ya mkataba wake kumalizika.

Farid hana namba chini ya kocha Miguel Gamondi tofauti, lakini alipokuwa chini ya Nasreddine Nabi alikuwa anamtumia katika maeneo mbalimbali kama winga na beki, na akawa anafanya vizuri.

Mwanaspoti lilipomtafuta Gamondi kuzungumzia ishu za usajili ndani ya kikosi hicho amesema sio muda sahihi wa kuzungumza nani anabaki au nani anaondoka kwa sababu ligi bado inaendelea na ana imani na wachezaji wake kuwa watatetea ubingwa.

“Tuna mechi zaidi ya tano unataka nizungumzie suala la kuondoka kwa wachezaji, sio sahihi na haiwezi kuwa na afya kwangu hasa kipindi hiki tunapambana kusaka matokeo ili tuweze kutetea taji la ligi,” amesema.

Related Posts