Tanga. Watu wanne wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa wakidaiwa kufanya vurugu kwenye vituo vya kupigia kura kwenye Wilaya za Pangani na Tanga mjini, wakati upigaji kura ukiendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Novemba 27, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi amesema wananchi hao wamekamatwa kwa kosa la kuchana nyaraka za Serikali wakati wa uchaguzi huo ukiendelea.
Kamanda Mchunguzi aliwataja waliokamatwa kwenye tukio hilo kuwa ni Mohamed Selemani Juma (40) Mkazi wa Mwanzange Jijini Tanga na Devotha Sostenes Mpari (48) mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mivumoni, Kata ya Bushiri Wilaya ya Pangani kwa kosa la kuchana nyaraka za uchaguzi.
Wengine ni Yosefa Komba (38) na Sikujua Almasi (38) wote wakazi wa Genge Wilayani Muheza kwa kosa la kufanya fujo kwenye kituo cha kupigia kura.
Amesema kuwa taratibu za kiuchunguzi zinaendelea kukamilishwa ikiwa ni pamoja na kupata maelezo ya watu walioshuhudia matukio hayo, ili hatua nyingine za kisheria zifuate.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linawataka wananchi kufuata wajibu wao wa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuhakikisha mchakato unafanyika kwa utulivu na amani,” amesema Kamanda Mchunguzi
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kuvuruga uchaguzi.