Haya hapa mafanikio ya kudhibiti mfumuko wa bei Tanzania

Katika ulimwengu wa uchumi wenye mabadiliko yasiyotabirika, Tanzania imefanikiwa kwa jambo la kipekee, imeweza kudhibiti mfumuko wa bei kwa kiwango cha kuridhisha. Hadi Septemba 2024, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.1 pekee, kiwango ambacho kinabaki ndani ya lengo la Benki Kuu ya Tanzania, hali inayozidi kuleta utulivu kwa familia na wafanyabiashara.

Mafanikio haya ni matokeo ya mikakati thabiti, sera muafaka, na mazingira mazuri yaliyojengwa kwa uangalifu mkubwa.

Mfumuko wa bei, kama moto, unaweza kuwa rafiki au adui. Ukiwa umedhibitiwa, unaweza kuleta manufaa, lakini ukiachwa, unaweza kuharibu. Kwa muda mrefu nchi yetu imeweza kudhibiti “moto” huo wa kiuchumi kwa kuwa na sera madhubuti za kifedha na kibajeti zinazochukuliwa kwa umakini mkubwa. Matokeo yake, bei zinapanda, lakini katika wastani unaokadiriwa, sio kwa kasi ya kuweza kudhuru ukuaji wa uchumi. Na ndio mfumuko wa bei wenye utulivu.

Benki Kuu ya Tanzania imekuwa nguzo ya mafanikio haya, ikitumia sera zake za fedha kama chombo makini cha kudhibiti hali. Kwa mfano, kwa kuweka kiwango cha riba cha Benki Kuu kuwa asilimia 6 na kusimamia kwa uangalifu mzunguko wa fedha, Benki imeweza kusawazisha mahitaji ya uchumi.

Mathalani, katika msimu wa juu wa kilimo mwezi Septemba 2024, Benki Kuu iliongeza Sh2.1 trilioni katika mzunguko ili kukidhi mahitaji ya fedha za wanunuzi wa mazao. Hatua hii ilihakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelea bila kusababisha mfumuko wa bei kupanda.

Kwa mujibu wa taarifa ya BoT kuhusu mwenendo wa uchumi kwa mwezi Oktoba 2024, bei za chakula, ambazo mara nyingi huchochea mfumuko wa bei, zimechangia pakubwa katika utulivu huu.

Mfumuko wa bei wa chakula umeshuka hadi asilimia 2.5, hali inayotokana na upatikanaji mzuri wa mazao muhimu kama mahindi na mchele. Utulivu wa bei za chakula unapunguza makali ya kibajeti kwa familia nyingi, jambo linalowapa nafuu katika nyakati za mabadiliko ya uchumi.

Hata hivyo, sekta zote hazijafaidika kwa usawa. Mfumuko wa bei wa nishati umeongezeka hadi asilimia 11.5, kutokana na kupanda kwa gharama za kuni na mkaa, ambazo bado ni chanzo kikuu cha nishati kwa kaya nyingi.

Hii inaonyesha pengo muhimu katika vita dhidi ya mfumuko wa bei. Wakati sehemu nyingine za uchumi zinanufaika na utulivu, nyingine zinaweza kuwa zinahisi mvuke wa moto wa gharama za maisha, hasa jamii za kipato cha chini.

Utulivu wa bei si takwimu ya kiuchumi tu, ni uti wa mgongo wa maisha ya kila siku. Mkulima anayepanga msimu ujao wa kupanda mazao au mzazi anayebuni bajeti ya ada ya shule hutegemea kutabirika wa bei. Wakati mfumuko wa bei unadhibitiwa, unaleta ujasiri si tu kwa masoko, bali pia kwa mustakabali wa watu, si jambo la kubeza.

Hata hivyo, changamoto bado zipo mbele. Kwa mfano mivutano ya kisiasa kimataifa, mabadiliko ya tabianchi, au kubadilika kwa bei za bidhaa za nishati.

Ili kujenga msingi thabiti zaidi, Tanzania inapaswa kuimarisha mifumo ya kilimo, kupanua chaguo za nishati mbadala, na kuboresha ufanisi wa masoko ili kupunguza mfumuko wa bei wa chakula na nishati.

Udhibiti wa mfumuko wa bei si mafanikio ya muda mfupi, bali ni vita vya muda mrefu vinavyohitaji uangalizi na maono. Mafanikio ya sasa ya Tanzania ni ushuhuda wa nguvu ya sera nzuri na ushirikiano madhubuti.

Kama methali ya Kiswahili inavyosema, “Usione vyaelea, vimeundwa”, usifikiri mafanikio huja kwa bahati; hujengwa kwa juhudi. Changamoto sasa ni kudumisha usawa huu na kuhakikisha manufaa yake yanafika kila kona ya jamii.

Related Posts